BARAZA la Madiwani wa Manispaa ya Dodoma limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dokta John Magufuli kwa hatua yake ya kuivunja rasmi iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na kwamba hatua hii ni maamuzi muhimu na sahihi kwa maendeleo ya Manispaa na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla.
Wajumbe wa Baraza hilo likiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo Jumanne Ngede walikutana jana kwenye ukumbi wa Manispaa kwa ajili ya Mkutano Maalum wa kuzungumza na vyombo vya Habari na kutoa tamko rasmi la kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo.
Walidai hatua hiyo itafungua milango kwa wawekezaji wengi kuwekeza Dodoma kutokana na taratibu za upatikanaji na umiliki wa ardhi kuboreshwa chini ya Manispaa, ikiwemo utolewaji wa hati za umiliki wa ardhi za miaka 99 badala zile za miaka 33 zilizokuwa zikitolewa na iliyokuwa CDA.
Mei 15 mwaka huu, Mheshimiwa Rais Dokta John Magufuli alisaini tamko la Amri ya Rais la kuivunja iliyokuwa CDA baada ya kujiridhisha kuwa kwa sasa hakuna mahitaji ya kuwa na mamlaka hiyo iliyoanzishwa kwa Amri ya Rais mwaka 1973, na kwamba shughuli, mali, na watumishi 284 wanakuwa chini ya Manispaa ya Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.