BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lapitisha kwa kauli moja makisio ya Mpango na Bajeti ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi 128,278,555,369 kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ruzuku ya mishahara na matumizi mengineyo.
Makisio hayo yalipitishwa katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akiwasilisha rasimu ya makisio ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Mchumi wa Jiji la Dodoma, Francis Kaunda aliyataja kuwa ni jumla ya shilingi 128,278,555,369. “Kati ya fedha hizo shilingi 55,128,229,369 ni mapato ya ndani, shilingi 59,082,835,000 ruzuku ya mishahara, shilingi 1,005,792,000 ruzuku ya matumizi mengineyo na shilingi 13,061,699,000 ruzuku ya miradi ya maendeleo” alisema Kaunda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa bajeti hiyo inakwenda kuangazia ukamilishaji wa miradi viporo. “Katika kikao cha Baraza la Chama kilituelekeza tuandae orodha ya miradi viporo yote ya Jiji la Dodoma na kuigawa kwenye Tarafa na madiwani wajiridhishe kama ndiyo miradi viporo wanavyovitambua wao. Tutaitembelea miradi viporo yote na kuifanyia tathmini na kuona jinsi ya kuikamilisha” alisema Mafuru.
Akiongelea vyanzo vya mapato ya ndani, alisema kuwa watavianisha na kuviwekea mikakati ya ukusanyaji wake. Alisema kuwa ofisi za kata zitapewa fursa ya kusimamia mapato katika maeneo yao ili kutoa ufanisi.
Akiongelea upelekaji wa fedha za kutekeleza miradi katika Kata, alisema kuwa madiwani watapewa taarifa. “Kwenye upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo katika Kata, waheshimiwa madiwani watataarifiwa mapema katika hatua za awali ili waweze kushauri miradi yenye matokeo ya haraka ianze kutekelezwa. Wakati wa utoaji wa fedha tuwataarifu madiwani ili washauri” alisema Mafuru.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.