MKUTANO wa dharura wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma umepitisha kwa kauli moja kuhamisha eneo la Ikulu ya Chamwino kwenda Jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi.
Akihitimisha mkutano huo wa dharura Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa Baraza la Madiwani limepitisha mapendekezo ya Kata tatu za Chamwino, Buigiri na Msanga kuingia Jiji la Dodoma. Mapendekezo mengine ni kugawanya Jimbo la uchaguzi la Dodoma mjini, kuongeza tarafa moja na kuunda halmashauri mbili za Manispaa.
Awali akiwasilisha taarifa ya mapendekezo ya kuhamisha eneo la Ikulu ya Chamwino na kuhamia Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mjumbe wa kamati ya kupitia taarifa ya mapendekezo ya kuhamisha eneo la Ikulu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na kwenda Halmashauri ya Jiji la Dodoma, William Alfayo alisema kuwa kamati ilikuwa na hadidu za rejea tatu. Alizitaja kuwa ni kupitia Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma kuangalia Kata za Wilaya ya Chamwino zilizoingizwa na matumizi yake. Nyingine aliitaja kuwa ni mapendekezo, athari na utatuzi wake katika utekelezaji wa kuhamisha Ikulu kwenda Jiji la Dodoma na Mpango kazi wa utekelezaji.
Alfayo alisema “kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma 2019-2039 ambao unatekelezwa hivi sasa, kata za Jiji la Dodoma ambazo zipo ndani ya eneo la Ikulu ni Chahwa kwa Mtaa wa Muungano na Kata ya Mtumba Mitaa ya Vikonje A na Vikonje B. Aidha, mpango huo kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, kata tatu ambazo ni kata za Msanga, katika Kijiji cha Msanga, Kata ya Chamwino katika Kijiji cha Chamwino na Kata ya Buigiri katika Kijiji cha Buigiri na sehemu ya Kijiji cha Chinangali II zipo ndani ya eneo la Ikulu”
Ikumbukwe kuwa sehemu kubwa ya eneo la Ikulu ipo upande wa Jiji la Dodoma kwa ukubwa wa hekta 2,249 sawa na ekari 5,557 kati ya jumla ya hekta 3,429 sawa na ekari 8,469.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.