BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha shilingi 1,654,000,000/= kwa ajili ya mradi wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi Tanzania Bara (BOOST), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu kwa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026.
Shukrani hizo zilitolewa na Mwenyekiti, Jamal Ngalya katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kuwasilisha taarifa za utekelezaji za robo ya tatu (Januari-Machi) 2023 kwenye Kata uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Ngalya ambaye ni Naibu Meya wa Jiji la Dodoma alisema kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi 1,654,000,000/= kwaajili ya mradi wa BOOST ili kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu. “Sisi waheshimiwa madiwani tusiposimama kumshukuru huyu Mama tutakuwa tunatenda dhambi kubwa sana. Jiji la Dodoma tumepewa shilingi 1,654,000,000/= kwaajili ya mradi BOOST fedha zilizogawanywa katika kata nne ambazo ni Msalato, Hombolo Makulu, Ipagala na Mnadani”.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Hombolo Makulu, CP. Gideon Nkana alisema “…ni ukweli usiopingika Rais wetu amefanya mambo makubwa sana katika nyanja mbalimbali kwa muda mfupi alioingia madarakani. Tunampongeza sana kwa juhudi anazozifanya kwaajili yakuliletea taifa hili maendeleo hasa katika sekta ya elimu. Niwaombe waheshimiwa madiwani wenzangu, tukazisimamie fedha hizi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili zilete matokeo chanya kwa taifa letu”.
Naye Diwani wa Kata ya Majengo, Shufaa Ibrahim alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha alizotoa kwaajili ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji. “Kwakweli Mama anatusafisha sisi wanawake wenzake, tunamshukuru na kumpongeza sana mwanamke mwenzetu ambaye anaonesha msimamo wake. Sisi kama viongozi wanawake tupo nyuma yake katika kuhakikisha fedha hizi alizozitoa zinatumika ipasavyo. Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, hekima na busara na sisi viongozi tuwe na afya njema ili tuweze kuwaongoza watu waliotupa dhamana ya uongozi” alisema Ibrahim.
Mradi wa BOOST ulianzishwa na Serikali chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia ukisimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ukilenga kuimarisha sekta ya elimu ya msingi nchini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.