BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma ‘limemwaga’ sifa nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri hiyo zaidi ya shilingi bilioni 2.97 za maendeleo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Wakizungumza katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika Oktoba 27, 2021 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jiji hilo, baadhi ya Madiwani waliochangia taarifa ya mapokezi ya fedha hizo walisema ni njambo la kihistoria kupata mgao wa fedha nyingi kama hizo kutoka Serikali Kuu.
Diwani wa Kata ya Kilimani Neema Mwaluko alisema katika kumbukukumbu zake Halmashauri hiyo haijawahi kupokea fedha nyingi za maendeleo kwa wakati mmoja kama ilivyotokea sasa huku akitoa wito kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kumuombea Mhe. Rais Samia ili azidi kufanya mambo makubwa zaidi katika kukuza uchumi wa nchi.
Akichangia hoja hiyo, diwani wa Kata ya Chang’ombe Mhe. Bakari Fundikira alisema Mhe. Rais Samia amekuwa akiipa kipaumbele cha aina yake Halmashauri hiyo ya Makao Makao ya Nchi kwa muda mrefu ukiwemo ujenzi wa miradi mikubwa kama uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato, barabara za lami za mzunguko na Mji wa Serikali, na sasa ujenzi wa madarasa takribani 143 ya shule za sekondari yenye gharama ya shilingi bilioni 2.86 jambo ambalo halijawahi kutokea katika awamu zote za utawala wa nchi.
Naye diwani wa Kata ya Zuzu Mhe. Awadhi Abdallah alisema, alichokifanya Mhe. Rais Samia ni jambo la kihistoria na la kukumbukwa daima kwani kupata madarasa 143 kwa wakati mmoja haijawahi kutokea, huku akitoa wito kwa watendaji wa jiji la Dodoma kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo ndani ya muda alioelekeza Mhe. Rais Samia.
Katika mpango huo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepatiwa kiasi hicho cha fedha cha zaidi ya shilingi bilioni 2.97 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na kampeni ya chanjo dhidi ya UVIKO-19.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.