BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma limekutana leo Aprili 25, 2019 na kujadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu (Januari mpaka Machi, 2019) kwa mwaka wa fedha 2018/2019, huku kikihudhuriwa pia na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri hiyo, Watendaji wa Kata, na Wananchi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika robo ya tatu, Katibu wa Baraza hilo ambaye pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi alisema kuwa, Halmashauri hiyo kupitia Idara ya Mipango Miji, Ardhi na Maliasili imepunguza kwa kiasi kikubwa migogoro sugu ya ardhi, na kwamba Jiji kwa kushirikiana na wadau wengine wanaendelea kutekeleza majukumu ya Upangaji, Upimaji na uthamini wa ardhi.
‘Kwa kipindi cha mwaka mmoja, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza kupima viwanja zaidi ya laki moja, tofauti na iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ambayo kwa miaka yote ilipima viwanja elfu 69 tu, na kati ya viwanja hivyo tulivyopima tumetenga viwanja zaidi ya 2000 kwa ajili ya kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma’ Alisema Kunambi.
Kunambi alisema kuwa, endapo Halmashauri hiyo ingeviuza viwanja hivyo kwa gharama nafuu kabisa, Jiji lingeweza kupata mapato ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.9, fedha ambazo zingeweza kutumika kujengea Shule, Zahanati na kuboresha huduma nyingine za Jamii.
"Kuna baadhi ya maeneo wananchi wamepewa maeneo bure kwa kulipishwa ada ndogo tu za kisheria, pesa ambayo inakwenda moja kwa moja Serikali Kuu na kuna maeneo mengine wananchi wanalipia kidogo sana, wapo wananchi waliokaa kwenye maeneo ya shule, maeneo ya wazi na hifadhi za barabara, ambapo ili wananchi hao wapishe maeneo hayo ya Serikali tunahitaji viwanja 1170 kwenye kata ya Ipagala pekee kwa ajili kuwapa kama mbadala, ila kwa awamu ya kwanza tumetenga viwanja 600, Makulu 600, Chang’ombe 200 , Nkuhungu 286, na maeneo mengine tumefanya hivyo...kwa kufanya hivyo, tunaamini tunaweza kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika Halmshauri ya Jiji la Dodoma" Alisema Kunambi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Dodoma ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Antony Mavunde alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeingia katika historia kutokana na kufanikiwa kutatua migogoro mingi ya Ardhi iliyokuwepo kwa muda mrefu.
Mavunde alisema, tangu Mwaka 2015 aliahidi kutatua migogoro ya Ardhi akiwa kama Mbunge na kuhakikisha Wananchi wanauziwa viwanja kwa bei nafuu, jambo ambalo limefanikiwa ambapo sasa wakazi wa Dodoma wanaweza kupata viwanja kwa gharama nafuu ambayo si rahisi kupata sehemu nyingine.
Wakichangia taarifa ya Katibu, Madiwani wengi waliopata nafasi walimpongeza Mkurugenzi wa Jiji Kunambi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Halmashauri kwa jitihada madhubuti wanazozifanya kwani zimechangia kufanya vema katka ukusanyaji wa mapato na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa na Jiji kwa wananchi wake, huku wakisifu ushirikiano mzuri uliopo kati ya Madiwani na Watendaji wa Halmashauri na kusisitiza ushirikiano na umoja huu uendelee kwa maslahi mapana ya Halmashauri na ustawi wa watu wa Jiji la Dodoma kwa ujumla.
Wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakifuatilia Mkutano wa Baraza hilo lililokutana Aprili 25 Mwaka huu kujadili taarifa za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2018/2019. Kutoka kushoto ni Diwani wa Viti Maalum Mhe. Elisi Kitendya, Diwani wa Viti Maalum Mhe. Joan Mazanda (Katikati) na Diwani wa Kata ya Zuzu Mhe. Awadhi Abdallah.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.