HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imezindua Baraza Lake la wafanyakazi, huku likitakiwa kutoa ushirikiano kati yake na mwajiri, ili kuleta ufanisi kwenye sehemu ya kazi ikiwemo kuondokana na malalamiko yanayoweza kusababisha kuwepo kwa migogoro mahali pa kazi.
Aidha, viongozi wa baraza hilo wameshauriwa kutatua changamoto na kutetea masilahi ya wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa kujituma na kuiwezesha halmashauri kuwa na tija na ufanisi zaidi.
Ushauri huo umetolewa na Afisa kazi wa Mkoa wa Dodoma Neema Dickson alipokuwa akizungumza baada ya kulizindua baraza kwenye mkutano uliokuwa na ajenda ya kuwachangua Katibu na Naibu katibu wa baraza hilo la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lililofanyika leo tarehe 29/01/2022 katika Ukumbu Mkuu wa Jiji la Dodoma.
Dickson akizungumza kwenye baraza hilo amelitaka kuwa na ushirikiano kati ya mwajiri, viongozi na wafanyakazi ili kuepuka migogoro isiyo kuwa na tija inayokwamisha utendaji wa kazi ambayo imekuwa ikijitokeza baina ya pande zote.
“Ninyi viongozi ambao mpo kwenye baraza la wafanyakazi wa Jiji ninawaomba muwe sehemu ya kutatua changamoto ikiwemo na kutetea maslahi ya watumishi pamoja na mikataba inayotolewa na waajiri” alisema.
Afisa huyo ameyataka mabaraza ya wafanyakazi kuwa na wabinifu wa kuanzisha miradi kwa ili kuongeza mapato.
Kwa upande wa Afisa Utumishi Mkuu wa Jiji la Dodoma, Gerald Ruzika amelitaka baraza la wafanyakazi wa Jiji kufanya kazi na mwajiri wao kwa kushirikiana ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za kila siku halmashauri hiyo.
Alisema ushirikiano, upendo na kujituma kwenye utendaji wa kazi ndiyo njia mojawapo itakayoweza kufanikisha kuboresha maslahi kwa wafanyakazi, hivyo amewataka kuwa kitu kimoja kwenye utendaji wa majukumu yao sehemu ya kazi.
Naye Katibu mpya wa Baraza la wafanyakazi wa halmashauri ya jiji Dodoma aliyechaguliwa katika mkutano huo, Denis Gondwe, alisema kuwa pamoja ya majukumu mengine waliyonayo, wanapaswa kuhakikisha maslahi ya watumishi yanalindwa ikiwapo kuthibiti migogoro baina yao na mwajiri kwa kuhakikisha kuwa inatatuliwa katika meza ya majadiliano na kupata ufumbuzi sahihi.
Gondwe alisema kuwa baraza la wafanyakazi la Jiji litahakikisha inafanya kazi kwa kuwatetea ili haki ya kimsingi ya mfanyakazi iweze kupatikana huku pia kwa upande wake mtumishi akizalisha kwa malengo ya kuiletea halmashauri maendeleo.
Imeandikwa na Peter Mkwavila DODOMA
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.