BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma limepitisha kwa kauli moja bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika mkutano uliofanyika Februari 17, 2022 katika ukumbi mkuu wa mikutano wa Jiji hilo ambapo zaidi ya shilingi bilioni 100.9 zimeidhinishwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru aliwasilisha taarifa yenye muhtasari wa bajeti hiyo na kuwajulisha wajumbe wa baraza hilo kuwa pamoja na mambo mengine, vipaumbele kwa mwaka huo wa fedha itakuwa kumalizia viporo vya miradi ya maendeleo, kuimarisha huduma hususan maeneo ya pembezoni pamoja na kuimarisha miundombinu katika sekta muhimu zaidi ikiwemo elimu na afya.
Wajumbe wa baraza hilo wakiongozwa na Mstahiki Meya wa jiji hilo Prof. Davis Mwamfupe kwa pamoja waliunga mkono hoja iliyotolewa na Diwani wa Kata ya Chang’ombe Mheshimiwa Bakari Fundikira aliyewataka wajumbe kuipitisha bajeti hiyo kwa asilimia mia moja kwani imesheheni mambo muhimu na vipaumbele vya msingi kwa wakazi wa Halmashauri hiyo.
Kufuatia kuwasilishwa kwa hoja hiyo, Mstahiki Meya Prof. Mwamfupe aliwahoji wajumbe ambao kwa kauli moja waliunga mkono kupitishwa kwa bajeti hiyo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti, Meya huyo alitoa angalizo kuwa Ofisi ya Mkurugenzi ihakikishe bajeti husika inatekelezwa kama ilivyoandaliwa ili iwe na tija kwa Halmashauri na kuzidi kuliweka Jiji la Dodoma katika ubora zaidi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.