BENKI ya Dunia kupitia kwa Wataalamu wake wa ushauri na tathimini wamepongeza utaratibu unaotumiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kusimamia ujenzi wa miradi mikubwa na kuweka mazingira rafiki na mahusiano mazuri baina ya Wakandarasi na Wananchi kwenye hatua za Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati (TSCP) katika Jiji la Dodoma, ikiwa ni pamoja na mradi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kisasa na Soko Kuu katika eneo la Nzuguni Jijini humo.
Haya yamebainishwa na ujumbe wa wataalamu washauri na tathimini ya maendeleo ya Ujenzi kwa kushirikiana na wasimamizi wa miradi ya Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati (TSCP) kutoka TAMISEMI katika ziara ya siku mbili ya kutembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ili kuona hatua iliyofikiwa kwa kuzingatia muda wa ujenzi na masharti ya ujenzi yaliyoafikiwa kwenye mikataba.
“Kwa kweli katika miradi tuliyotembelea nchi nzima, Jiji la Dodoma mmetufurahisha sana, mmeonyesha mshikamano wa pamoja katika usimamizi na ndiyo maana mmefanikiwa kutatua changamoto kwa kiasi kikubwa” alisema Beatrice Mchome ambaye ni Afisa Mazingira na Mshauri wa Masuala ya Kijamii kutoka TAMISEMI.
Mratibu wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Jiji la Dodoma, Mhandisi Emmanuel Manyanga amesema Serikali imesaini mikataba ya ujenzi wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na kwamba kuna miradi mikubwa inayoendelea kujengwa ikiwemo Kituo Kikuu cha mabasi, Soko Kuu, Kituo cha maegesho ya malori, Barabara za Lami za mitaa, vivuko vya waenda kwa miguu, Bustani ya mapumziko na burudani, pamoja vizimba katika maeneo ya kukusanyia takangumu.
Manyanga alisema miradi mingine ni ujenzi wa Mtandao wa barabara katika mitaa mbalimbali zenye urefu wa kilometa 26.7 kwa kiwango cha lami, ufungaji wa taa za barabarani zitakazotumia mwanga wa jua, na ujenzi wa mtaro mkubwa wa maji ya mvua wenye urefu wa kilometam 6.5 katika eneo la Ilazo – Ipagala.
“Benki ya Dunia huleta wataalamu kukagua miradi inayojengwa kwa uwiano na fedha walizotoa kugharamia miradi hiyo na kuangalia Maendeleo, Changamoto, Kushauri pale inapobidi na kuangalia mapungufu ili kuongeza ufadhili katika miradi husika.” alisema Mayanga
Miradi iliyotembelewa na Ujumbe huo kutoka Benki ya Dunia na Wizara ya TAMISEMI ni pamoja na Soko Kuu la Kisasa, na Kituo Kikuu cha mabasi inayojengwa na Mkandarasi wa Kitanzania kupitia kampuni ya Mohamed Builders Ltd eneo la Nzuguni, Ujenzi wa Bustani ya Mapumziko na burudani linalojulikana kama ‘Chinangali Park’ na Dampo la Kisasa la kuhifadhi takangumu kwa teknolojia ya kuzika ardhini (Sanitary Landfill) lililopo eneo la Chidaya nje kidogo ya Jiji.
Miradi yote imenza kujengwa Julai Mosi Mwaka 2018, ikiwa ya thamani ya shilingi bilioni 77.8 za Kitanzania na inatarajiwa kukamilika Mwezi Oktoba, 2019.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.