HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imewataka wafanyabiashara waliopangishwa vibanda vya biashara katika eneo la Mji Mpya maarufu kama Mambo Poa kuacha tabia ya kupangisha vibanda hivyo kwa watu wengine kinyume na mkataba na kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Marufuku hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo na Vijana wa Halmashauri hiyo Asha Vuai wakati wa kikao na wafanyabiashara hao kilichofanyika leo Agosti 26, 2021 katika eneo hilo ambapo aliwaeleza kuwa Halmashauri hiyo inamtambua mpangaji aliyesaini mkataba wa pango na ndiye anayetakiwa kufanya biashara na kutumia nyaraka zake ikiwemo leseni ya biashara na siyo kugeuka dalali au mmiliki na kupangisha mtu mwingine.
“Haitatokea Halmashauri ikupangishe kibanda halafu na wewe ugeuke mmiliki upangishe kwa mfanyabiashara mwingine, hiyo haikubaliki na ukibainika utachukuliwa hatua stahiki” alisisitiza Vuai.
Katika hatua nyingine, Halmashauri hiyo imewasilisha mapendekezo ya namna mpya ya kulipa kodi ya pango ambapo kuanzia sasa mfanyabiashara atalipa kodi kila baada ya robo ya mwaka wa fedha badala ya kulipa kila mwezi kama ilivyokuwa awali.
Akiwasilisha mapendekezo hayo kwa wafanyabiashara hao kabla ya kujadiliwa na kukubalika, Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hiyo Peter Malya alisema kuwa, menejimenti ya Jiji imependekeza kuja na mfumo huo ili kuwapunguzia wafanyabiashara hao adha ya kutumia muda wao mwingi kwenda kulipa kodi hiyo kila mwezi badala yake watalipa kwa mkupuo wa miezi mitatu.
“Kwa njia hii ya sasa itakuwa ni rahisi hata kulipa kwa mfumo wa kutumia namba ya malipo (Control Number) kwa sababu ndiyo maelekezo ya Serikali yanataka hivyo, meneja wa eneo hili atakuwa anapokea risiti tu baada ya mfanyabiashara kufanya malipo” alifafanua Malya.
Wakichangia katika hoja hiyo, baadhi ya wafanyabiashara walisema mfumo huo ni mzuri na wameupokea kwa ajili ya utekelezaji ili kuendelea kuhakikisha serikali inakusanya kodi kwa wakati na kwa wingi ili iwaletee wananchi wake maendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.