Na WAF - Dar es Salaam
Serikali imeazimia kutumia Shilingi Bilioni 161. 3 za Mfuko wa pamoja wa Afya kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha mifumo ya afya nchini ili kutoa huduma bora za afya ya msingi kwa wananchi sambamba na kupunguza vifo vya watoto vitokanavyo na uzazi na kuimarisha huduma za bima ya afya kwa wote.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, Julai 18, 2025, Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kusaini makubaliano (Side Agreement) kwa mwaka wa fedha 2025/26 baina ya Serikali ya Tanzania na Wadau wake tisa (9) wa Maendeleo wanaounga mkono Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund - HBF) – ambao ni Canada, Denmark, Ireland, Korea Kusini, Uswisi, Uingereza, UNFPA na UNICEF.
Amesema wadau wa maendeleo wameahidi kutoa jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 55.9 sawa na takribani Shilingi Bilioni 161.3 za Kitanzania kwa mwaka wa fedha 2025/26, fedha ambazo zitatumika kugharamia ununuzi wa dawa, vifaa tiba, na vifaa vya afya pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma bora za afya ya msingi, vituo vya afya, mikoa hadi ngazi ya taifa.
“Wadau wetu wa maendeleo wameridhishwa na kuimarika kwa huduma za afya ya mama na mtoto na hatua ya kuanzisha kwa Bima ya Afya kwa Wote, sasa tunakwenda kuongeza nguvu zaidi katika kudhibiti vifo vya watoto vitokanavyo na uzazi,” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amesema kupitia mipango, mikakati na vipaumbele vinavyowekwa na Serikali ya Tanzania katika matumizi madhubuti ya fedha ndio imekuwa chachu na kivutio kwa wadau kuongeza fedha za miradi ya maendeleo.
Amesema, Tangu kuanzishwa mfuko huo mwaka 1999, zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.3 sawa na takribani Shilingi Trilioni 3.2 zimeshatolewa kwa ajili ya kutekeleza Mipango Mkakati ya Sekta ya Afya.
Aidha kuanzia mwaka 2017, fedha zimekuwa zikipelekwa moja kwa moja kwenye vituo vya afya vya umma na zaidi ya vituo vya afya vya ngazi ya msingi 7,300 vimenufaika na fedha hizo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.