MBIO za Mwenge wa uhuru mwaka 2022 zilizofikia kilele tarehe 14 Oktoba 2022 mkoani Kagera, zimefanikiwa kurejesha fedha za mikopo kwa vijana kupitia mfuko wa Maendeleo ya vijana kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 2.2.
Moja ya ajenda ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 ilikuwa ni kuhakikisha fedha zote zilizorejeshwa na vijana waliopewa mikopo kupitia Mfuko huo na kupotelea katika ngazi za Halmashauri nchini zinarejeshwa katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu
Akiongea wakati wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako alisema serikali kuu kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka wa fedha 1993/1994 imekuwa ikitoa fedha za mikopo kwa vijana kupitia mfuko wa Maendeleo ya vijana.
"Vijana wetu walitumia fedha hizo katika shughuli zao za kiuchumi na kurejesha kwa wakati katika halmashauri zao. Lakini katika hali ya kustaajabisha baadhi ya halmashauri hizo hazikurejesha fedha hizo Serikali kuu, kama miongozo ya fedha hizo ilivyozitaka na hivyo kudhoofisha jitihada za Serikali Kuu kuwahudumia vijana. "
Prof. Ndalichalko alisisitiza kuwa, lengo la kuanzishwa kwa Mfuko huo ni kuwawezesha vijana wote nchini kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali.
Aidha alifafanua kuwa Kupitia utaratibu huo, vijana huwezeshwa kujitegemea, kupunguza umaskini wa kipato na kujiajiri wenyewe.
Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Julai mwaka huu imetoa muongozo mpya wa kutoa mikopo kupitia Mfuko huo, ambapo kwa sasa kijana mmoja anaweza kupewa mkopo huo kupitia Halmashauri, hiyo ikiwa ni tofauti na awali ambapo vijana walipata mikopo hiyo wakiwa katika vikundi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.