Na Getruda Shomi, DODOMA.
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imetenga shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kukarabati shule zilizopo kwenye Halmashauri hiyo ikiwa ni moja ya mpango wake wa kufanya maboresho ya kimiundombinu katika shule hizo ili kuendelea kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Joseph Mafuru wakati akijibu swali la papo kwa papo lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Makole Mhe. Omary Haji katika kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Chuo cha Mipango.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa ameshatoa maelekezo kwa Maafisa Elimu wa shule za msingi na sekondari kuanza mchakato wa manunuzi na kutafuta mafundi ili kuweza kukarabati shule hizo.
“Jiji limetenga zaidi ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya shule zake, kila shule iliyoingizwa kwenye bajeti itaboreshwa, nimeshatoa maelekezo kwa Afisa elimu shule ya sekondari na msingi waanze mchakato wa kuwatafuta mafundi, hivyo kama Makole ipo kwenye bajeti itafanyiwa kazi.” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Aidha, alisema kuwa kwa shule ambazo hazikuwekwa kwenye bajeti hiyo ya ukarabati zitatakiwa kufanyiwa kazi kwa kushirikisha na wadau wa maendeleo Jiji la Dodoma kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya Jiji hilo.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mkakati huo wa kukarabati shule za msingi na sekondari utaanza mwezi Agosti, 2021 ambapo bajeti ipo tayari na utekelezaji wake utaanza hivi karibuni huku akitoa wito kwa Madiwani kutoa ushirikiano wakutosha kipindi cha utekelezaji wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mafuru alijibu swali la Diwani wa kata ya Mbabala Mhe. Paskazia Mayala lililouliza Halmashauri amejipanga vipi kutoa elimu ya chanjo katika Kata za pembezoni, ambapo alijibu kuwa ”timu ya Madaktari na Wataalam wa afya itatembea kwenye Kata na maeneo yote yenye mikusanyiko ili kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kwa kina kwa sababu upotoshaji ni mwingi na Halmashauri inatambua uwepo wa changamoto hiyo.
Diwani wa Kata ya Makole Mhe. Omary Haji na waheshimiwa madiwani wengine wa Jiji la Dodoma wakifuatilia hoja zilizokuwa zikiwasilishwa katika Baraza la Madiwani la Jiji la Dodoma.
Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Jiji la Dodoma, Mhe. Jaffar Mwanyemba (kushoto), Mhe. Beatrice Ngerangera (katikati) na Mhe. Gideon Nkana (kushoto) kwa makini wakifuatilia mada wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mhe. Awadh Abdallah wa Kata ya Zuzu na Mhe. Amos Mbalanga wa Kata ya Kiwanja cha Ndege wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Jiji la Dodoma.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Dodoma, Sharifa Nabalang'anya ambaye ni Mkurugenzi mteule wa Halmashauri ya Njombe (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji wa Jiji la Dodoma, Shabani Juma ambaye ni Mkurugenzi mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika (kulia) wakiteta jambo na Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi wa Jiji la Dodoma, Albert Kasoga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.