Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepokea shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya elimu katika shule 19 ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora na salama.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na maafisa watendaji wa kata na wakuu wa shule za sekondari katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisema “nina taarifa ya kwamba tumepokea fedha shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya elimu katika shule 19 kwenye matundu ya vyoo na madarasa. kuna changamoto imekua ikitusumbua sana viongozi pamoja na wananchi. Kuna sehemu zina changamoto za elimu na hoja ni kukosekana pesa, sasa pesa zimekuja tutekeleze kukamilisha changamoto hizo ili tusiwe na sababu. Lengo la kukutana hapa ni kupanga kwa pamoja ni kwa namna gani tutaenda kutumia pesa hizo ili tutekeleze miradhi hiyo. Kwahiyo mpaka wiki ijayo tuone taarifa ni kitu gani kilichotekelezwa na muongozo wa taarifa ya matumizi ya fedha ziandikwe na zitawasilishwa katika vikao”.
Mkuu wa wilaya alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kutekeleza miradi ya elimu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Tangu program ya ukarabati wa shule kongwe, ujenzi wa madarasa na shule mpya, tumepokea zaidi ya shilingi 7,000,000,000 katika eneo hilo ni fedha nyingi mno. Nilishawahi kuzunguza huko nyuma kwa Hamashauri ya Jiji la Dodoma tuna mapato makubwa sana, Mheshimiwa Rais angeweza kusema hakuna haja na kuwapa pesa zaidi. Lakini bado alitupatia pesa ili tuweze kukamilisha miradi mbalimbali. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan na kumpongeza kwa kuendelea kutoa fedha hizo ili kuendeleza miundombinu ya elimu katika jiji letu” alisema Shekimweri.
Alielekeza kuundwa kamati tatu muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Alizitaja kamati hizo kuwa ni ujenzi, kamati ya manunuzi na kamati ya usimamizi. Kwa upande wa halmashauri waweke mfumo mzuri wa usimamizi na utendaji wa fedha hizi, aliongeza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.