MFUKO wa Afya ya Jamii Ulioboreshwa unalenga kumhakikishia mwananchi uhakika wa afya njema kupitia matibabu kwa mwaka mzima wilayani Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi alipokuwa akizindua kampeni ya uhamasishaji mkubwa wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa jana katika mtaa wa Mahomanyika katika kata ya Nzuguni jijini Dodoma.
Katambi alisema kuwa watu wengi wanatembea na magonjwa sababu hawaendi hospitali kupima kwa kuogopa kutozwa fedha. “Siku ugonjwa ukizidi utakuta huwezi kwenda kufanya kazi na kutafuta fedha na wala huwezi kutibiwa. Nataka kuwaambia ukiwa na bima ya afya kwa familia ya watu sita unafaida mara mia nane tofauti na mtu asiyekuwa na bima hiyo. Huku ukienda tu hospitali unalipa shilingi 6,000 ukipewa rufaa ya kwenda mjini unalipa shilingi 15,000” alisema Katambi.
Mkuu wa Wilaya aliwakumbusha wananchi kuwa Rais Dkt. John Magufuli wakati akiomba kura alisema kuwa ataboresha huduma za afya. Miongoni mwa utekelezaji wa ahadi hiyo ni uboreshaji wa huduma za CHF ambapo unalipia shilingi 30,000 na kuhudumiwa watu sita kwa mwaka mzima. Katika kuonesha serikali inawajali wananchi wake, kila anayelipia shilingi 30,000 kwa CHF serikali inaongeza tena shilingi 30,000.
Akiongelea faida za CHF iliyoboreshwa, Katambi alisema kuwa inamuwezesha mwananchi kupata huduma bora katika eneo lake. “Serikali imeendelea kujenga na kuboresha zahanati, vituo vya afya na hospitali na kulipa mishahara madaktari na wataalam wa sekta ya afya ili wananchi waweze kupata huduma bora” alisema Katambi. Faida nyingine ya CHF aliitaja kuwa ni upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao.
“Ndugu zangu, napenda kuwahakikishia kuwa ukiwa na bima ya afya unakuwa umejiandaa muda wowote katika eneo la matibabu. Niwaombe wananchi wa Mahomanyika tujisajili katika bima ya afya. Huna sababu ya kukopa unapougua au kuuguliwa, tujipange sasa” alisisitiza Katambi.
Awali mratibu wa CHF katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga alisema kuwa lengo la maboresho ya CHF ni kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanajiunga na mfuko huo ambao utawasaidia kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Mratibu huyo alisema kuwa dhumuni la kuboresha CHF ni kutenganisha watoa huduma za tiba na usimamizi wa bima, kuweka mfumo wa bima, kuongeza idadi ya wananchama, kutoa mfumo wa utambulisho utakaowezesha huduma kupatikana kwa mwanachama akiwa sehemu yeyote katika Mkoa wa Dodoma.
CHF iliyoboreshwa imebuniwa na wataalam wa mradi wa HPSS- Tuimarishe afya ikiwa imetumia uzoefu wa mifuko ya bima ya afya ya jamii kutoka India pamoja na matokeo ya tafiti zilizofanywa ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi (mwenye kipaza sauti) akiongea na wananchi wa Mahomanyika alipokuwa akihamasisha jamii kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.