Rawan Dakak ni mshichana wa Kittanzania mwenye umri wa miaka 18 mzaliwa wa Arusha, akiwa tayari ameshaweka rekodi ya kipekee ya kupanda milima mirefu sita duniani.
Mwezi ujao, anatarajia kutimiza ndoto ya kupanda mlima mrefu duniani, Mlilma Everest wenye kimo cha mita 8,848 kutoka usawa wa bahari, katika eneo la Mahalangur, ambalo ni sehemu ya milima ya Himalaya, inayotenganisha mipaka ya mataifa ya Nepal na China.
Kuna usemi ‘usione vyaelea, ujue vimeundwa.’ Binti Rawan alianza kupanda mlima nchini akiwa na umri wa miaka 12 tu, baada ya kujiunga na timu ya shule ya upandaji milima, alikopatiwa elimu, ujuzi na taarifa mbalimbali za milima duniani. Baada ya kupata mafunzo yaliyomwingia kwa tija, msichana huyo alivutiwa sana na mchezo wa kupanda na akajikuta, ushiriki wake unamwekea rekodi ya kupanda milima mirefu kutoka katika mabara yote duniani.
ILIKUWAJE?
Rawan alisema ni uamuzi wake binafsi uliomsukuma kujitosa katika mchezo huo milimani, na alihakikisha haungiliani na kuharibu masomo yake, katika lengo la kupata ufaulu. Anabainisha kuwa ndoto yake imekuwa ya kweli na mpaka sasa ameshapanda milima sita katika mabara manne akipeperusha bendera mbili katika kila kilele alichofikia, moja ya nchi yake Tanzania na ya pili amani ya dunia.
Binti huyo anasema, lengo lake kuu ni kufikisha ujumbe wa kutaka amani duniani, kuhamasisha maendeleo kwa wanawake na vijana wa rika lake, akiwataka wajitahidi kutimiza ndoto zao na kufahamu chochote wanachikiwekea nia kinawezakana. Akitaja baadhi ya milima aliyokwishapanda ni wa nyumbani Mlima Kilimanjaro, wenye urefu wa mita 5,895, mwingine ni Elbras uliopo nchini Russia barani Ulaya wenye urefu wa mita 5,648.
Mingine anayoitaja ni Aconcagua uliopo nchini Argentina, Amerika Kusini wenye urefu mita 6,962; Carstenz Pyramid, uliopo Indonesia barani Asia, wenye urefu wa mita 4,884 na Vinson Massin, ulio mrefu zaidi katika bara Antartica jirani na nchi ya Chile, ukiwa na urefu wa mita 4,892.
ALIVYOJIANDAA
Rawan anasema, siri ya mafanikio yake ni kwamba, kila mara alipotaka kupanda milima, alitakiwa kufanya mazoezi kwa saa 20 kila wiki, yanayompa uwezo wa kubeba mzigo wake wenye kilo 35, katika hali ya hewa ya baridi chini ya nyuzi joto sentigredi 30 akinuia kutimiza ndoto ya kuupanda Mlima Everest.
Kijana huyo anasema, ni aina ya mazoezi yanayowavutia wengine kushirikiana na tayari kuna wenye vifaa vya kupanda mlima vyenye uzito wa kilo 30 na wanafanya mazoezi ya kuhimili upandaji mlima. Katika mazoezi hayo, ameshapanda miwili mkoani Arusha, ukiwamo Mlima Meru wenye kimo cha mita 4,562; Ruwenzori nchini Uganda, una mita 5,109; Mlima Kazbegi wenye kima cha mita 5,033, nchini Russia.
Anaeleza imani yake kwamba, atakapofanikiwa kufika kilele cha Mlima Everest wenye kima cha mita 8,848, ataingia katika rekodi kuwa mwanamke wa kwanza mwenye umri mdogo duniani kupanda mlima huo. Mbali na hilo, anasema atakuwa Mtanzania wa kwanza kupanda mlima huo na kuvunja rekodi kwa kupanda milima yote mirefu iliyopo katika mabara saba ya dunia.
"Nafanya mazoezi ya ndani kwa saa 20 kwa wiki, yanayonipa uwezo wa kubeba mzigo wenye kilo 10 hadi 15 na kuvuta mwingine wenye uzito hadi kilo 25,” Binti huyo akazia kuwa “Mazoezi mengine ninayoyafanya ni kupanda mlima katika hali ya baridi, mazoezi haya yamenilazimu kupanda mlima Kilimanjaro uliopo Tanzania wenye mita 5,895 na mlima wenye baridi kali wa Kazbek.”
Anataja milima mingine anayofanyia mazoezi ni yenye kimo cha mita 3,820 ukiwamo Ararat wenye mita 5,137 nchini Uturuki; Mlima Kenya (mita 4,985); na Qurnat wa Lebanon wenye (mita 3,088). “Hii nimepanda kwa ajili ya mazoezi ya kupanda mlima mrefu kuliko yote duniani," anasisitiza Rawan.
Historia inaonyesha watu wa kwanza kufikia kilele walikuwa Edmund Hillary wa New Zealand na Sherpa Tenzing Norgay wa nchini Nepal, Mei 29, 1953, jambo ambalo kijana wa Kitanzania anaamini utamwingiza katika historia ya kuwa mwanamke kijana na Mtanzania wa kwanza kufika kilele cha Mlima Everest.
Rawan anakiri ni safari ngumu, ila anaamini ataimaliza vyema, akiwa na rai kwa Watanzania kumwombea safari yake ikamilike, atimize ndoto hiyo ya kitaifa kufikia kilele cha milima saba duniani. Hadi sasa ameshapanda milima sita.
MAMA YAKE
Mama yake mzazi anaitwa Hala, anasema alipogundua ndoto ya mtoto wao, waliamua kumuunga mkono kwa kumpa ushirikiano wa kila hatua aliyofanya. Anasema alikuwa na malengo ya kupanda milima yote mikubwa duniani na hadi sasa kufikia mafanikio aliyoyataja, akithibitisha kauli ya mwanawe, kwamba alianza akiwa na umri wa miaka 12 na hivi sasa anajiandaa kwenda kupanda mlima mrefu zaidi duniani.
Hala anaongeza; “Wazazi wenzangu napenda kuwaambia mtoto akiwa na ndoto yake tusiipuuze bali tumsaidie kufikia anapotaka.”
KUTOKA TANAPA
Kamishna wa Hifadhi Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) Dk. Allan Kijazi, anampongeza kijana huyo wa kike kwa kuweza kupanda orodha ya milima hiyo, ikiwamo wa nchini Kilimanjaro hali akiwa na umri mdogo. Ahadi yake katika nafasi ya Tanapa, ni kumpa ushirikiano wa kutosha katika utimizaji wa ndoto yake, huku akibainisha pindi kijana huyo atakaporejea nchini kutoka katika safari yake ya kupanda mlima huo, atakuwa balozi mzuri wa kuutangaza mlima Kilimanjaro duniani.
Dk. Kijazi anasema, kijana huyo wa kike akirudi wataanzisha programu atakayoifanya kupita katika shule mbalimbali nchini, kuwahamasisha wenzake kupanda Mlima Kilimanjaro.
Chanzo: www.ippmedia.com
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.