Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Siasa ya Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma imeridhishwa na kazi inayofanywa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho wilayani Dodoma na kuelekeza fedha za serikali kusimamiwa vizuri.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Dodoma, Charles Mamba alipoongoza Kamati ya Siasa ya Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa mawili, mabweni mawili, viti na meza 60 katika Shule ya Sekondari ya wasichana Bunge iliyopo Kata ya Kikombo jijini Dodoma.
Mamba alishauri miti kupandwa na kutunzwa katika shule hiyo ili kutengeneza mazingira bora na yakuvutia. “Shule hii ni yetu, tuisimamie vizuri ili wanafunzi wanaokuja kusoma hapa wajue na kuthamini mchango wetu katika maendeleo ya shule. Lazima msimamie vizuri fedha hizi za serikali. Wote tunatambua kuwa kuwa mama yetu Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri, tuisimamie huku katika maeneo yetu ili matunda yaonekane. Mheshimiwa DC Shekimweri kazi zako nazikubali, ni nzuri, hongera sana” alisema Mamba.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alielekeza mabweni mawili katika shule hiyo yakamilike kwa wakati ili wanafunzi wayatumie na kuagiza kuimarishwa kwa usalama katika mabweni hayo. Aidha, aliagiza kichomea taka kiwe karibu na mabweni ya wasichana.
Awali Afisa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Prisca Myalla alisema kuwa serikali kupitia Mradi wa kuboresha Shule za Sekondari (SEQUIP), ilitoa shilingi 244,200,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, vyumba viwili vya madarasa na kununua viti na meza 60. “Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua hiyo muhimu ya kuongeza fursa kwa wasichana kusoma masomo ya sayansi kwa utulivu” alisema Mwalimu Myalla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.