BUNGE la Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika (Common Wealth Parliamentary Association in Africa-CPA) linatarajia kujenga makao makuu yake katika Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji ya Bunge la Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika, Justin Muturi alipoongoza kamati ya uwekezaji ya Bunge hilo kutembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuangalia fursa za uwekezaji na kuzungumza na waandishi wa habari jana.
Muturi ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kenya alisema kuwa CPA inapanga kujenga jengo la makao makuu yake na kuhamia Dodoma. Alisema kuwa kamati yake imetembelea na kuridhishwa na eneo yatakapojengwa makao makuu ya jumuiya hiyo katika ukanda maalum wa uwekezaji Njedengwa Jijini Dodoma.
Muturi alisema kuwa, pamoja na ujenzi wa makao makuu hayo, CPA inapanga kujenga hoteli ya kifahari yenye hadhi ya nyota tano katika Jiji la Dodoma.
“Niishukuru Serikali na wananchi wa Tanzania kwani muda mrefu hapo zamani walitupatia sehemu ya kujenga ofisi ya CPA katika nchi hii, hata wale ambao hatukuwepo wakati ule tunaendelea kuwa na shukrani nyingi” alisema Muturi.
Alisema kuwa hoteli hiyo ya kifahari inatarajiwa kugharimu dola za kimarekami milioni 30.
Mwenyekiti huyo alielezea kufurahishwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuupanga mji katika ubora unaovutia.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe aliwakaribisha kuwekeza Dodoma. “Mnakaribishwa kama taasisi kuja kuwekeza katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kama mtu binafsi pia mnakaribishwa kuwekeza hapa Dodoma…nataka kuwahakikishia kuwa Dodoma tuna ardhi ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji” alisema Prof. Mwamfupe.
Vilevile, aliwakaribisha wabunge wa Jumuiya ya Madola (Afrika) kufanya mkutano wa mwaka Jijini hapa.
Prof. Mwamfupe aliwataarifu wabunge hao kuwa, Halmashauri yake inautaratibu wa kupanga maeneo, kuyapima, na kuyapelekea huduma ili wananchi na wawekezaji waweze kuwekeza na kuendeleza maeneo hayo bila vikwazo.
Ujenzi wa hoteli hiyo ya kifahari inatarajiwa kugharimu dola za kimarekani milioni 30 hadi itakapokamilika, wakati matarajio ya ujenzi kuanza ni mwaka 2019/ 2020.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.