BUNGE limeridhia azimio la kubadilisha hadhi ya sehemu ya Pori la Akiba la Ugalla lililopo mkoani Tabora kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla.
Pia limeridhia azimio la kubadilisha hadhi ya sehemu ya Pori la Akiba la Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi. Pori hilo linapatikana katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Shinyanga likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 7,000.
Maazimio hayo mawili yaliwasilishwa bungeni jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, ambaye aliliambia Bunge kuwa serikali imefikia uamuzi huo ili kuimarisha na kuendeleza uhifadhi wa maliasili.
Alisema lengo hilo pia linalenga kuhifadhi wanyamapori, mimea na mazalia na makuzio ya samaki na viumbe wengine wa kwenye maji na kuongeza Pato la Taifa, kwa msingi kuwa ubadilishaji hadhi wa sehemu ya mapori hayo kutasababisha hifadhi hizo kuwa kivutio cha utalii.
Kuhusu ubadilishaji hadhi ya sehemu ya Pori la Akiba la Ugalla yenye ukubwa wa kilomita za mraba 3,865 kati ya kilometa za mraba 5,000 za pori zima kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla, Dk Kigwangalla alisema hatua hiyo itaimarisha uhifadhi wa bioanuwai.
Alizitaja bioanuai hizo kuwa ni za wanyamapori, mimea na mazalia na makuzi ya samaki na hivyo kuongeza utalii wa ndani, kukuza uchumi wa jamii inayozunguka hifadhi, utafiti na kutoa elimu ya vitendo kwa wanafunzi na wananchi watakaotembelea hifadhi hiyo.
Kuhusu Pori la Akiba la Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi, alisema hatua hiyo itaimarisha ulinzi na kujenga mazingira bora kwa ajili ya kuendeleza utalii katika ukanda wa Magharibi.
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Catherine Ruge, alisema kambi hiyo inashauri serikali kuangalia upya uwapo wa mamlaka tatu za serikali zinazofanya shughuli za uhifadhi zinazofanana na hivyo kuliongezea Taifa mzigo.
Chanzo: Tovuti rasmi ya Habarileo (www.habarileo.co.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.