MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Felista Bura amewataka wanawake nchini kushiriki katika shughuli zitakazowezesha kujipatia kipato, huku akiwasisitiza kuachana na dhana ya kuwategemea wanaume kwa kila kitu katika kujipatia mahitaji yao ili kuweza kujenga jamii imara na yenye maendeleo.
Aliyasema hayo wakati akitoa hotuba katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Machi 8 mwaka huu yaliyofanyika katika ngazi ya Mkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkonze jijini hapo.
Bura alisema kuwa, usawa wa 50-50 kati ya wanawake na wanaume hauwezi kupatikana kama wanawake wataendelea kuwa na dhana ya utegemezi, lakini wakiamua kufanya kazi wataweza kujikwamua na dhana hiyo katika utekelezaji wa kaulimbiu isemayo “kizazi cha usawa kwa Tanzania ya sasa na ya baadae”.
“Kumekuwa na desturi ya wanawake kutokufanya shughuli za kujiingizia kipato na kutegemea wanaume kutekeleza jukumu hilo, usawa tunaouhitaji tutaupataje wakati hata kazi hatutaki kufanya, wakati umefika sasa wa wanawake kubadilika, kundi hili la wanawake ambao wanaishi hivi wanatuharibia malengo yetu ya kujikwamua kiuchumi, tunaendelea kudharaulika na kuonekana hatuwezi kwa ajili yao.
“Wakati umefika sasa wa wanawake kufanya maendeleo kwa kutumia kipato chetu wenyewe, upendeze kwa hela yako mwenyewe, usimtegemee mumeo kwa kila kitu, fanya bidii katika kujipambania na kujiwezesha mwenyewe usisubiri hadi uwezeshwe, hautaweza kujikomboa kuendea usawa endapo hata mahitaji yako mwenyewe unashindwa kujitimizia unasubiri hadi ufikiriwe na mtu mwingine,” alisema Bura.
Mbunge huyo pia aliitaka jamii kuondokana na mila kandamizi ikiwemo tabia ya wanaume kuchukua pesa zote baada ya mavuno kwa kushirikiana na wake zao kwa madai kuwa wao ndiyo vichwa na mihimili ya familia hivyo wana haki ya kuamua chochote wakati wowote.
“Kuna tabia pia kwa wanaume, ambao wanatumia kama silaha kumdidimiza mwanamke kwa kuwa tu amepewa nguvu na mila na desturi, kuna wanawake wanafanya kazi mno lakini hawafaidi matunda ya kile wanachokifanya, baada ya mafanikio wanaume ndo watu wanofanya starehe na kufuja mali bila hata kuwapa wanawake waliotafuta pamoja, tabia hizi zikomeshwe, wanawake wapatiwe stahiki zao kama wafanyavyo kazi.
“Nawashauri wanawake wenzangu, tuanzishe miradi itakayotuibua kiuchumi, kwani tutakuwa tumeshaondokana na vyote vinavyotukwamisha kimaendeleo, kuna mikopo ya Halmashauri tuunde vikundi tuwezeshwe kupitia asilimia nne ya mikopo hii tujiinua wenyewe kiuchumi”, alisema mbunge huyo.
Mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilikopesha jumla ya zaidi shilingi Bilioni 1.825 kwa vikundi 353 vya wanawake, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali Kuu la kila asilimia nne ya mapato ya ndani ya kila Halmashauri kuwapatia mikopo isiyo na riba wanawake.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.