Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma imefurahi kuona wakazi wa Kata ya Zuzu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakinufaika na shughuli za uvuvi katika bwawa la Zuzu.
Akielezea thathimini ya Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Dodoma baada ya kutembelea bwawa hilo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Meja Mst. Johnick Risasi alisema kuwa kamati yake imefurahia kuona wakazi wa Kata ya Zuzu wakinufaika na bwawa hilo. Aidha, aliishauri halmashauri kufanya utafiti wa jinsi ya kuliendeleza bwawa hilo ili liwe na tija zaidi kwa wananchi na kuiwezesha halmashauri kupata mapato pia.
Nae Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma, Sophia Kibaba alishauri kuwa kina cha bwawa hilo kiongezwe ili kuongeza uhakika wa upatikanaji Samaki. “Mwenyekiti, nashauri kuongeza kina cha bwawa la Zuzu ili kupata samaki wengi zaidi. Upatikanaji wa samaki wengi utapunguza kuagiza samaki kutoka nje ya Dodoma na kupunguza gharama kwa wananchi wetu, wakati huohuo kuwahakikishia mlo bora na kukabiliana na changamoto ya lishe” alisema Kibaba.
Akiwasilisha taarifa ya bwawa la Zuzu, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Gratian Mwesiga alisema kuwa bwawa hilo ni muhimu. “Bwawa hili lilianza kama mbuga kwa miaka mingi ambapo wakazi wa maeneo jirani walilitumia kulima Mpunga. Zamani kwenye mbuga hii kulikuwa na miti mingi hivyo maji yalikuwa yanatuama na kukauka. Baadae wananchi walikata miti yote na kuendelea kulima Mpunga. Baada ya kukata miti, maji hayakuendelea kutuama kwa muda mrefu, yalijaa wakati wa mvua na baadae kukauka” alisema Mwesiga.
Mkuu huyo wa idara alisema kuwa bwawa hilo lina jumla ya wavuvi 15 na wote wamelipa leseni ya uvuvi kwa mwaka 2021. “Samaki wanaopatikana kwenye bwawa hili ni Kambale na Perege” alisema Mwesiga.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa uvuvi katika bwawa hilo, Omary Kagusa alisema kuwa vijana katika kata hiyo hawakuwa na elimu ya uvuvi wa kutumia mitumbwi. Alisema kuwa walisaidiwa kupata elimu hiyo kwa kushirikiana na wataalam wa uvuvi kutoka maeneo mengine.
Mwenyekiti wa CCM Dodoma Mjini, Meja Mst. Johnick Risasi (mwenye shati la kijani) na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Rukia Bakari (kushoto) wakimsikiliza Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Gratian Mwesiga akitoa maelezo huu ya bwana na shughuli za uvuvi katika bwawa la Zuzu wakati Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma ilipofanya ziara katika Kata ya Zuzu.
Mwenyekiti wa CCM Dodoma Mjini, Meja Mst. Johnick Risasi (kushoto) akitoa nasaha zake mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma na wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua miradi katika Kata ya Zuzu Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.