Na. Dennis Gondwe, CHANG’OMBE
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Chang’ombe kimefurahishwa na jinsi diwani wa kata hiyo anavyohamasisha na kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuifanya kuwa ya kuigwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Chang’ombe, Bashiri Iddy alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa Chilewa katika Kata ya Chang’ombe kwenye mkutano wa hadhara.
Iddy alisema “tunaposema Diwani wa kata hii Bakari Fundikila anafanya kazi katika kata yake kwa weledi na uaminifu tuendelee kumuamini tunamaanisha tumeridhishwa na utendaji kazi wake. Leo tunavyosema amefanya kazi ya ujenzi wa kituo cha Polisi, amefanya kazi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Chang’ombe, amefanya kazi ya ujenzi wa masoko mawili Soko la Mavunde na lile la Hamvu, amefanya kazi ya kufungua barabara, amefanya kazi ya kuboresha elimu katika shule zetu siyo tunatania. Ni kazi ambazo kila mmoja wetu anaziona na anaweza kuzielezea. Kile kituo cha Polisi kinachojengwa pale ukubwa, ubora, sifa na uwezo kwa kituo hicho tunaongelea jitihada za Diwani Fundikila”.
“CCM Kata ya Chang’ombe tunasema Diwani Fundikila anakuwa ni kijana wa mfano, anakuwa ni kiongozi wa mfano. Leo kwa ubora wa utendaji kazi wake, Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuna nafasi inahitaji watu watatu makini na katika wale watu watatu yeye ni mmoja wao. Kwa nini ni mmoja wao hii ni kwasababu ya ubora na kazi anazofanya katika kata yake” alisema Iddy kwa kujiamini.
Mwenyekiti huyo alipongeza ushirikiano baina wenyeviti wa mitaa na diwani. “Ushirikiano wenu unanipa ujasiri na nafasi ya kuwatetea kwa jinsi mnavyofanya kazi. Hata mkichukua fomu nikiwa nikiwepo nitazipigania. Sitakubali kufanya mabadiliko ya viongozi kwa sifa za akili za kupenda watu, yaani unampenda mtu kwa sababu anajua kuongea na anajua kucheka lakini kwenye kazi hakuna kitu” alisema Mwenyekiti wa CCM Kata ya Chang’ombe.
Chama cha Mapinduzi Kata ya Chang’ombe kinafanya ziara ya kikazi katika Matawi yote ya chama hicho kukagua uhai wa chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kusikiliza kero za wananchi na kuwashukuru wanachama wake kwa kuchagua uongozi wa CCM Kata ya Chang’ombe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.