Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa ujenzi wa jengo la kisasa la wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) ili waweze kufanya shughuli zao katika eneo rasmi na salama.
Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kisasa la Machinga jijini Dodoma tarehe 13 Januari, 2022.
Mbanga alisema “pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa ushauri kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Mkuu wa Mkoa aliona Machinga wanatakiwa kuwa katika eneo zuri. Pongezi kwa Mkurugenzi wa Jiji kwa kutoa fedha nyingi kujenga jengo la Machinga ili wafanye kazi kwa staha”.
Aidha, aliwataka Machinga kuwa wazalendo kwa halmashauri yao na serikali yao kwa ujumla. “Tunatamani kuona Machinga wanatoka katika umachinga na kuwa wafanyabiashara wakubwa. CCM tutaendelea kuunga mkono juhudi za Rais na Serikali kwa ujumla. Rai kwa wilaya nyingine katika Mkoa wa Dodoma kuwatafutia Machinga maeneo mazuri ya kufanyia shughuli zao” alisema Mbanga.
Naibu Meya, Emmanuel Chibago alitoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa na ofisi yake kuendelea kuliunga mkono Jiji la Dodoma. “Hii inalifanya Baraza la Madiwani kuwa makini kumuunga mkono Rais kwa kuhakikisha Machinga wanafanya shughuli zao katika maeneo rafiki. Kwa niaba ya madiwani tupo pamoja” alisema Naibu Meya Chibago.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzile alisema kuwa Machinga wameshirikishwa katika mchakato wa utafutaji wa eneo na ujenzi wa jengo la kisasa la Machinga. “Rai yangu, Machinga tuwe wazalendo kwa nchi yetu, tusiingize watu wasiohusika katika mradi huu. Tukibaini anayetaka kuvuruga mpango huu hatutamvumilia. Walengwa ni wale Machinga 3,313 tuliowasajili.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alifanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kisasa la Machinga akiambatana na Katibu Tawala Mkoa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, viongozi wa Chama cha Mapinduzi na maafisa waandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.