Na. Dennis Gondwe, MIYUJI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kimewataka madiwani kufanya mikutano ya hadhara na kuwaeleza wananchi utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kata.
Agizo hilo lilitolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Miyuji B iliyopo Kata ya Miyuji jijini Dodoma.
Mbaga alisema “niendelee kuwasisitiza viongozi wa CCM lakini na viongozi wa kuchaguliwa madiwani na wenyeviti wa mitaa wafanye kazi ya kwenda kuwahabarisha wananchi kwenye mikutano ili wafahamu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewajengea shule kama hii na miradi mingine mingi ya maendeleo katika maeneo tofauti. Nimpongeze Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini anaendelea kufanya kazi kubwa ya kuwasogezea huduma wananchi”.
Aidha, aliwashukuru wajumbe wa kamati ya siasa kwa kuendelea kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025. “Mnafanya kazi nzuri ya kuisimamia serikali. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma pia amekuwa msaada mkubwa kufuatilia mradi huu lakini hakuishia hapa amekuwa msimamizi wa miradi yote ya Jiji la Dodoma. Nimshukuru na kumpongeza sana Mkuu wa Shule, Gerson Maige kwa kazi nzuri aliyoifanya amekuja kusimamia shule jirani. Maige ni mkuu wa shule ambayo ipo jirani kwa sababu kata hii haikuwa na shule ya sekondari, tunakushukuru sana kwa majengo mazuri na usimamizi mzuri” alisema Mbaga.
Wakati huohuo, alilipongeza Jiji la Dodoma kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Jiji mpo vizuri, miradi yenu ni bora kabisa na imara kabisa. Ninaimani itatunzwa vizuri ili vizazi vijavyo vitakuja kuitumia miundombinu hii na kusimulia kuwa kazi nzuri ilifanywa na watangulizi” aliongeza Mbaga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.