Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma imeshauri Kamati za Maendeleo za Kata kuwaalika viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya kata katika vikao vya maendeleo ili kupata majibu ya hoja zinazoulizwa na wananchi.
Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma, Meja Mst. Johnick Risasi wakati alipoongoza kamati hiyo kutembelea kituo cha kuzalisha Maji Mzakwe.
Meja Mst. Risasi alisema kuwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) imefanya kazi kubwa ya kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji. DUWASA imejenga na kuongeza miundombinu ya upatikanaji wa maji na kuwasogezea wananchi huduma hiyo, aliongeza. “CCM inaagiza watu wote wanaopitiwa na miundombinu ya Maji wanufaike na huduma ya Maji kama watu wa maeneo mengine. Hii ni sera ya Maji. Watu hao wakinufaika na huduma hiyo watashiriki kikamilifu katika ulinzi wa miundombinu hiyo” alisema Meja Mst. Risasi.
Katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na taarifa sahihi za upatikanaji wa huduma ya Maji, Mwenyekiti huyo ambae pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma alishauri uongozi wa kata kuwa wanawaalika viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya kata katika vikao vya Kamati za Maendeleo za Kata. Ushiriki wa viongozi hao utawawezesha kuwa na taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi ya Maji na usambazaji wa huduma ya Maji unaotekelezwa katika maeneo yao. Taarifa hizo zitawasaidia kutoa ufafanuzi kwa wananchi yanapoibuka maswali juu ya huduma ya Maji, aliongeza.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Sebastian Warioba alisema kuwa mamlaka yake imekuwa ikishirikishwa katika baadhi ya vikao vya kata na mitaa kwenda kuelezea miradi inayotekelezwa na hali ya upatikanaji huduma ya Maji. Alisema kuwa DUWASA wapo tayari wakati wowote kushiriki katika vikao hivyo ili kutoa elimu na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya shughuli wanazotekeleza Dodoma mjini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma, Meja Mst. Johnick Risasi (wa kwanza kulia) na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Dodoma wakisikiliza taarifa ya mradi wa maji kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Sebastian Warioba (mwanye Kaunda suti).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.