MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuwahudumia wananchi wa Makao Makuu ya nchi.
Kauli hiyo aliitoa muda mfupi baada ya kuapishwa rasmi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma tukio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma leo.
”Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kwa kuniamini na kunipa hii nafasi kubwa na ngumu kwelikweli lakini naamini amenipa nafasi hii baada ya ushauri wa vyombo vingi na yeye mwenyewe kuona kwamba huyu kijana anaweza akakimbia katika kasi anayoitaka. Na mimi kupitia vyombo vya habari niseme nitakwenda kwa kasi anayoitaka” alisema Mkurugenzi Mafuru kwa kujiamini.
Alisema kuwa malezi yanayoonekana yametokea kwa viongozi waliomtangulia akimtaja Mkurugenzi aliyepita Godwin Kunambi kuwa ni mfano wa kuigwa. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi huyu amepewa kipawa cha kutengeneza watu. ‘CMT’ yangu ni mashahidi kwamba wote tulikuja na tabia zetu lakini ametutengeneza, ilikuwa ngumu mwanzoni kufanya nae kazi lakini ametuelekeza hadi tukaenda pamoja. Kuna maneno alikuwa anayasema kwenye vikao ambayo tumeanza kuyaona, kwamba ninyi wote ninaofanya nanyi kazi ni muhimu na mtakuwa viongozi, yameanza kuonekana” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Zoezi la kuapishwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma lilifanywa na Mkuu wa Mkoa na kushuhudiwa na Yasmin Bakari aliyemwakilisha Kamishna wa Maadili kutoka Sektretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Kessy Maduka, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na waandishi wa habari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.