MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema kuwa kupatikana kwa vifaa vipya vya kisasa vya upimaji ardhi kwenye halmashauri hiyo, kuanzia sasa hawataingia tena mikataba na makampuni binafsi ya upimaji ardhi.
Mafuru alisema hayo wakati wa kupokea na kuzindua vifaa hivyo vya kisasa vya upimaji ardhi vilivyonunuliwa kwa gharama ya shilingi milioni 240 kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alisema kuwa baada ya Jiji kupata vifaa vyake gharama za upimaji itakuwa Sh 120,000 tu ambapo awali gharama za upimaji kwa makampuni binafsi ya upimaji ilikuwa ni shilingi 250,000.
Aidha, Mafuru alisema kuwa baada ya upatikanaji wa vifaa hivyo ni mategemeo yao sasa kutoingia mikataba na makampuni binafsi ya upimaji ardhi na makampuni yanayoendelea na kazi hiyo mara baada ya kazi zao kumalizia itakuwa imekwisha.
"Makampuni binafsi yamekuwa yakilalamikiwa na kusababisha migogoro mingine ya ardhi na lawama kutupiwa halmashauri ya jiji. Viwanja vilikuwa vinagawanywa vidogo vidogo, ili kuongeza faida na kwenye maeneo mengi kulikuwa kunaibuka migogoro kila siku." alisema Mafuru
Aliongeza kuwa awali Jiji lilikuwa na mahitaji makubwa ya upimaji viwanja na lisingeweza kufanya kazi hiyo peke yake ndipo wakaalika makampuni binafsi, lakini mwisho wa siku walizalisha migogoro mingine na Halmashauri kunyooshewa vidole.
Alisema walikuwa na mikakati mingi ya kuimarisha shughuli za upimaji ardhi na mwaka 2019 walinunua magari matatu na mwaka 2020 walinunua tena magari matatu.
Kwa uwepo wa vifaa hivi, sasa tunauwezo wa kupima viwanja 300 kwa siku na tutakwenda kupima maeneo ambayo upimaji ulisimama kwenye maeneo mbalimbali ndani ya halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Bihawana, Gawaye, Hombolo na maeneo mengine ya pembezoni ambayo upimaji ulisimama. Upimaji huo utafanyika kwa gharama nafuu.
Akifafanua zaidi, Mkurugenzi huyo alisema, sasa wako kwenye taratibu za kununua mitambo kwa ajili ya kufungua barabara ili kufanya Dodoma kuwa mji uliopangwa kuliko miji yote.
"Tunaenda kufungua barabara na kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya ardhi.” Alimalizia Mkurugenzi Mafuru.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri alisema vifaa hivyo kama vitatumika vizuri vitapunguza changamoto.ya upimaji katika maeneo mengi.
Alisema wakati Jiji linakabidhiwa iliyokuwa Mamlaka.ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kulikuwa na mahitaji ya viwanja 20,000 na kufikia sasa kazi kubwa imefanyika. "Jiji kupata seti sita zenye uwezo wa kupima viwanja 300 kwa siku sawa na viwanja 9,000 kwa mwezi ni jambo la kupongezwa," alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
"Ufanisi wa utendaji ni matokeo ya vitu vingi, tusijidanganye tukiwa na vifaa vizuri ndio tumemaliza, kwenye Idara ya ardhi sasa wana vifaa vya kutosha kusiwe na kisingizio, tuna uwezo wa kupima viwanja vingi hatutegemei tena migogoro kutoka kwa wananchi," alisema Shekimweri.
Naye Kaimu Mkuu wa idara ya Mipango miji Jiji la Dodoma Amelye Chaula, akitoa taarifa ya upatikanaji wa vifaa hivyo, alisema kuwa hivi sasa itawaondolea gharama ya kulipia makampuni ambayo ilikuwa ikiongezeka kila wakati.
Pia itaondoa malalamiko kutoka kwa wananchi yanayotokana na upimaji wa makampuni ambayo yalikuwa yakipima viwanja vidogo vidogo ili kuongezea faida.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe akizungumza wakati wa hafla hiyo
Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru akizungumza wakati wa hafla hiyo
Baadhi ya wadau wakifuatilia uzinduzi wa vifaa hivyo
Mkuu wa Wilaya Jabir Shekimweri akipata maelezo ya jinsi vifaa hivyo vinavyofanya kazi kutoka kwa mkuu wa kitengo cha upimaji Enock Katete
Baadhi ya vifaa vya upimaji ardhi vilivyonunuliwa na Jiji kwa gharama ya shilingi milioni 240
Mkuu wa wilaya Jabir Shekimweri akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Jiji wakiongozwa na Meya Mstahiki Prof. Davis Mwamfupe na Mkurugenzi wa Jiji Joseph Mafuru baada ya uzinduzi wa vifaa hivyo vya upimaji ardhi
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.