Katika kuunga Mkono juhudi za Serikali za kuendelea kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unayosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19), Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (Children's Dignity Forum - CDF) limekabidhi vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tisa na laki sita vitapelekwa kwa Afisa Elimu Msingi na Sekondari kwa ajili ya kugawa katika shule ambazo ziko katika sehemu ya mradi wa shirika hilo, Ofisi ya Mganga Mkuu wilayani humo (DMO), Ofisi ya Mkuu wa Wilaya (DAS), Dawati la jinsia na watoto Polisi na Mahakama ya Wilaya.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Afisa Tarafa wilayani humo Albert Mwalyego ambaye amepokea vifaa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri, Meneja Utekelezaji wa miradi ya CDF Evance Rwamuhuru amesema vifaa hivyo ni kwa ajili ya kupambana na janga la Corona wilayani humo na ni muendelezo wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na ugonjwa huo.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya mkuu wa wilaya Mpwapwa, Albert Mwalyego Afisa Tarafa wilayani humo amelishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada huo kwani utawasaidia kwa kiasi kikubwa huku akisema kuwa ni muhimu watu wakaendelea kuchukua tahadhari kubwa kama ambavyo wataalamu wa afya wamekuwa wakishauri.
Kwa upande wa Mganga Mkuu Wilayani humo (DMO) Dkt. Archard Rwezahura amesema licha ya kuwa hali ni nzuri katika nchi, lakini ni vizuri zaidi tahadhari ikaendelea kuchukuliwa huku akilishukuru shirika hilo kwa kutoa vifaa hivyo kwani vitawasaidia katika shughuli zao.
Akizungumzia kuhusu msaada huo, Afisa Elimu Sekondari bwana Nelson Milanzi amesema vifaa hivyo vitawasaidia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kujikinga na ugonjwa huo.
Shule za Sekondari ambazo zitanufaika na vifaa hivyo ni Kibakwe, Pwaga, Berege, Kimagai, Igovu na Mazae ilhali shule za Msingi ni Idunda, Kibakwe, Berege, Makulu, Pwaga, Munguyu, Lupeta, Bumila na Makutupa.
Vifaa vilivyotolewa ni Kipima joto (Thermo Scanner), Barakoa, Vitakasa mikono, Ndoo, Glavu, Maski, Aproni za matibabu, Spiriti, unga wa Chlorine, kikinga uso, Vifaa vya Kufanyia upasuaji na matanki ya maji yenye ujazo wa lita 500.
Meneja utekelezaji wa miradi ya Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto Evance Rwamhuru (kushoto) akimkabidhi ndoo ya kunawia Afisa Tarafa wa Wilaya ya Mpwapwa Albert Mwalyego (kulia).
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Archad Rwezahura (wa pili kulia) akielekeza namna ya uvaaji gauni la upasuaji wakati wa makabidhiano ya vifaa vya kujikinga na Corona vilivyotolewa na CDF.
Baadhi ya vifaa vilivyotolewa na CDF kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.