Chama cha Waendesha Baiskeli Tanzania (CHABATA) na kampuni ya Green Waste Pro kwa kushirikiana na Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamefanya usafi katika baadhi ya maeneo Jijini hapa ikiwa ni katika harakati za kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumza na mwandishi wetu kiongozi wa CHABATA Mkoa wa Dodoma Simba Alei, amesema kuwa wameamua kufanya usafi ili kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo kwa sababu Mwalimu alikua anapenda na kuthamini mazingira.
“Ili uendeshe Baiskeli ni lazima uwe na afya bora na huwezi kuwa na afya bora kama mazingira yanayokuzunguka ni machafu, hivyo tumeamua kufanya usafi ili kuhamasisha wananchi wengine kufanya hivyo ili kutunza afya zao” Alisema Alei.
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Ally Mfinaga amesema kuwa wamefurahi kupata ugeni huo ambao umeongeza hamasa kwa wadau wengine na wananchi kujitokeza kwa wingi kufanya usafi na kufanya Jiji hilo kuwa katika hali nzuri na ya kupendeza.
Mfinanga aliongeza kuwa wao kama Halmashauri wamekua na desturi ya kufanya usafi katika mitaa na barabara ndani ya Jiji hilo ili kuliweka Jiji katika hali ya usafi jambo ambalo linasaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko.
“Tuna timu ya watu ambayo inafanya kazi masaa yote tukishirikiana na kampuni ya usafi ya Green Waste ambao wamekua wadau wakubwa wa kuhakikisha Jiji hili linakua safi wakati wote, ndio maana maeoneo mengi ya Jiji letu ni masafi kutokana na mikakati tuliyojiwekea kwa kuzingatia kaulimbiu yetu ya Mita tano usafi wangu” Aliongea Mfinanga.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Kandarasi ya Usafi Jijini Dodoma ya Green Waste Stefano Damas amekishukuru CHABATA kwa uamuzi wao wa kuweka kambi Dodoma na kushiriki katika shuguli za usafi kwani kwa kufanya hivyo wameonesha mfano mzuri kwa vyama vingine vya michezo nchini kushiriki katika shuguli za kimaendelao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.