Na. Faraja Msibe, DODOMA
CHAMA cha Alliance for African Farmers (AAFP) kimeridhishwa na mchakato wa uteuzi wa wagombea uliofanywa na wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuuita kuwa ulikuwa shirikishi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Vijana wa Mkoa wa Dodoma wa Chama cha AAFP, Fredrick Mapua alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea, mapingamizi na maamuzi ya rufaa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mapua alisema “nimekuja kuzungumzia mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia uteuzi wa wagombea, mapingamizi na maamuzi ya rufaa. Nianze kwa kumshukuru sana Rais, mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya amejaribu sana kusimamia demokrasia nchini. Mchakato ulienda vizuri sana. Tulifanya vikao baina ya wasimamizi wa uchaguzi na vyama vya siasa kwa ajili ya kufanya uchaguzi kuwa huru na wa haki. Hivyo, mchakato ulikuwa shirikishi tangu awali. Kwa chama changu tulihudhuria vikao hivyo, nikiwepo mimi binafsi, tulikuwa tulipatiwa miongozo kila mjumbe nakala yake. Maelezo na kanuzi zilikuwa wazi. Wale wenye uwezo wa kusoma na kuandika walikuwa wanauwezo wa kusoma nakuelewa nini kilichokuwa kinahitajika na nini kilichokuwa hakihitajiki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Maelezo yalikuwa yanajitosheleza kwenye kanuni kama ulizifuata sidhani kama unaweza kuwa muanga wa wale walioenguliwa katika mchakato wa uchaguzi huu”.
Alisema kuwa kufuatia mchakato huo haki ilijaribu kutendeka na ilipatikana. Kwa wale walioona wameonewa fursa ya rufaa ilikuwepo. “Chama changu tulikaa na kujadili wapi tunamapungufu na wapi wenzetu wametuzidi ili tusionekane bado wadogo sana. Sisi tulifuata taratibu na kanuni zote. Hivyo, kwenye chama changu hakuna aliyeenguliwa kutokana na makosa madogo madogo kama walivyokuwa wakilalamika vyama tofauti kwenye mitandao ya kijamii. Kwa chama chetu wote tulikuwa makini na kulifuata maelekezo ya mwongozo” alisema Mapua.
Akiongelea amani na utulivu alisema kuwa ni wajibu wa vyama vya siasa. Alisema kuwa chama chake kimeweka mkakati kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu. “Sisi tunapenda amani, utulivu, siasa safi na salama. Hatupendi kuona watu wakiumia au kuharibikiwa mali kutokana na siasa. Ukiona mtu anatumia nguvu sana kutaka madaraka jiulize mara mbili” alisisitiza Mapua.
Katika hatua nyingine Katibu wa Chama cha Kijamii (CCK) Mkoa wa wa Dodoma, Abuutwahiru Iddi alisema kuwa mchakato wa kuteua wagombea ulifanyika vizuri ukiwa shirikishi. “Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa aliitisha vikao mbalimbali kwa lengo la kufanikisha zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. “CCK nayo ilishiriki kuhamasisha wananchi wake kuweza kuchukua fomu, zimejazwa na kurudishwa ofisi za serikali za mitaa kwa mujibu wa kalenda na ratiba. Mchakato umeenda vizuri na sasa tunajiandaa kufanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa tarehe 27 Novemba, 2024. Chama kinaendelea kuhamasisha wananchi ili kuelewa zaidi maana ya uchaguzi na waweze kujitokeza kupigia kura viongozi wanaowahitaji tofauti na kubaki nyumbani na wanapopatikana vongozi ambao hawawahitaji watabaki kulalamika kwa miaka mitano inayofuata” alisema Iddi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.