Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KATA za Chamwino, Mnadani, Tambukareli na Ipagala zimefanya vizuri zaidi katika ushiriki wa viongozi na wananchi kwenye mazoezi ya usafi wa Mazingira na upendezeshaji mji ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wa kulifanya jiji hilo kuwa usafi na la kuvutia kimazingira.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na udhibiti wa taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kuwasilisha taarifa za utekelezaji za robo ya tatu (Januari-Machi, 2023) kutoka kwenye kata uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kimaro alisema kuwa kuishi katika Mazingira safi na salama ni haki ya kisheria. “Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 4 kinafafanua kuwa kila mtanzania ana haki ya kuishi katika Mazingira safi, salama na ya kiafya. Halmashauri imekuwa na juhudi kubwa za kuhamasisha wananchi wake kufanya usafi wa Mazingira, kupanda maua na miti katika maeneo yao ili kuhakikisha yanapendeza” alisema Kimaro.
Alisema kuwa kikao cha Kamati ya Mipango miji na Mazingira cha Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichoketi tarehe 25 Aprili, 2023 kilipendekeza kutoa vyeti vya pongezi kwa mitaa iliyofanya vizuri katika ushiriki wa viongozi na wananchi kwenye usafi wa Mazingira. “Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaa iliyofanya vizuri ni Mwaja kutoka Kata ya Chamwino, Mtaa wa Karume kutoka Kata ya Mnadani, Mtaa wa Amani kutoka Kata ya Tambukareli na Mtaa wa Swaswa Halisia kutoka Kata ya Ipagala. Vigezo tulivyozingatia ni usafi wa mazingira kuzunguka nyumba, makazi na biashara, taasisi, mitaro ya maji ya mvua na maeneo ya wazi. Kikubwa zaidi ni ushawishi wa viongozi wa kisiasa hasa wenyeviti na mabalozi kushiriki kwenye usafi wa kaya na jumuiya” alisema Kimaro.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatekeleza mkakati wake wa kulifanya jiji hilo kuwa safi na lenye mandhari ya kupendeza kwa kuweka mkazo wa ushiriki wa wananchi katika kufanya usafi wa maeneo yao mita tano kuzunguka maeneo ya makazi na biashara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.