CHANGAMOTO ya upatikanaji wa maji safi katika Kata ya Hombolo nje kidogo ya Jiji la Dodoma inatarajiwa kuwa historia baada ya Halmashauri ya Jiji hilo kusaini mkataba wa mradi wa matengenezo ya miundombinu ya maji kwa fedha za mapato ya ndani.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hilo Godwin Kunambi jana alipokuwa akitoa maelezo mafupi ya mradi wa matengenezo ya miundombinu ya maji Hombolo Bwawani “A” kwa fedha za mapato ya ndani katika hafla ya utiaji saini mikataba iliyofanyika katika viunga vya Nyerere square jijini hapa.
“Halmashauri ya Jiji la Dodoma tunataka tatizo la maji Hombolo liwe historia ndiyo maana katika bajeti ya mwaka ujao wa Fedha (2019/2020) tumetenga shilingi bilioni 1.3 katika mapato ya ndani” alisema Kunambi.
“Mkataba utakaosainiwa leo wa shilingi milioni 690 unalenga matengenezo ya miundombinu ya maji Hombolo ili kuwahakikishia wananchi uhakika wa huduma ya maji safi” aliongeza Kunambi.
Akizungumzia mradi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Selemani Jafo aliutaja mradi huo kuwa unaenda kujibu matatizo ya wakazi wa Hombolo.
Wakati huo huo, Waziri Jafo amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin kunambi kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwaletea maendeleo wananchi.
“Nakupongeza sana wewe Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, wewe unafanya kazi sana, naomba Mungu asaidie ubaki hapa ili asije akaja mwingine akaharibu mazuri unayoyapanga” alisema Waziri Jafo.
“Dodoma ni Jiji pekee linaloongoza kwa pato ghafi katika Halmashauri zote nchini, kuna Halmashauri nyingine bajeti yake ni shilingi bilioni 33, mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma yanaweza kuendesha Halmashauri nyingine bila Serikali Kuu kuongeza fedha za uendeshaji” aliongeza Waziri Jafo.
Mkataba wa mradi wa matengenezo ya miundombinu ya maji safi katika Kata ya Hombolo Bwawani ‘A’ utatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani kwa kipindi cha miezi mitano kwa gharama ya shilingi milioni 690.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.