KIKUNDI cha Tujikubali walemavu kinachoendesha kiwanda kidogo cha kutengeneza viatu vya ngozi kinakabiliwa na changamoto ya masoko jambo linalosababisha kusua kwa marejesho.
Kauli hiyo ilitolewa na Mweka Hazina wa kikundi hicho, Pauleta Lesso alipokuwa akisoma taarifa fupi ya kikundi hicho kwa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma ilipofanya ziara ya kukitembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na kikundi hicho Mtaa wa Nzuguni “B”.
Lesso alisema “kikundi chetu kinachojihusisha na kiwanda kidogo cha utengenezaji viatu vya ngozi kwa sasa shughuli zinaendelea vizuri, japo bado tuna changamoto ya masoko inayopelekea kusuasua kwa marejesho ya mkopo wetu”.
Changamoto nyingine alizielezea kuwa ni miundombinu na usafiri wakati wa kutafuta masoko na kuuza bidhaa ni shida, alisema. “Changamoto nyingine ni kutawanyika kwa baadhi ya wanakikundi wenzetu kutokana na sababu zao binafsi na kupoteza uaminifu ndani ya kikundi” alisema Lesso.
Kuhusu mafanikio ya mradi, aliyataja kuwa wameweza kununua vifaa na malighafi kwa ajili ya kutengenezea viatu na kunufaika na mashine ambazo zilirahisisha kazi. “Mashine hizi ziliturahisishia kazi na kupelekea kupata fedha za marejesho na kujikimu kwa kila mwanakikundi. Hivyo, mkopo wa asilimia mbili ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya watu wenye ulemavu umeleta tija kwa walemavu. Watu wenye ulemavu wakishirikiana kwa pamoja huleta maendeleo chanya kwa kikundi, kila mwanakikundi na jamii kwa ujumla. Kupitia mkopo huu tumefanikiwa kujenga jengo dogo la ofisi yetu ambayo ipo kwenye hatua ya umaliziaji” alisema Lesso.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma, Meja Mst. Johnick Risasi aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata mikopo ya asilimia mbili kutoka mapato ya ndani. Alisema kuwa kitendo cha Halmashauri kuwakopesha watu wenye ulemavu ni kuonesha kuwajali watu hao. “Mheshimiwa Rais Samia anazungumzia usawa kwa watu wote. Watu wenye ulemavu wakiwezeshwa wanaweza kujiletea maendeleo. Ushauri, watu hawa watafutiwe sehemu nzuri na kuangalia jinsi ya kuwezeshwa kulipa pango. Huku wanapofanyia shughuli zao pamejificha sana” alisema Meja Mst. Risasi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma, Meja Mst. Johnick Risasi (aliyesimama) akitoa nasaha zake kwa wanakikundi cha Tunajikubali walemavu alipoambatana na kamati yake kutembelea miradi ya vikundi kutoka kwenye Kata za Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.