HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inakusudia kuchanja jumla ya watoto 90,999 ili kuwakinga na magonjwa ya Polio na Surua katika kampeni ya kitaifa ya chanjo inayoendelea nchi nzima.
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Gatete Mahava ofisini kwake alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika kuhamasisha wananchi kupeleka watoto katika vituo vya kutolea huduma ya afya ili kupata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Polio na Surua.
Dkt. Mahava amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatarajia kuchanja jumla ya watoto 90,999 wenye umri chini ya miaka mitano. “Chanjo ya Surua itahusisha watoto wenye umri kuanzia miezi tisa hadi miezi 59 (Umri chini ya Miaka mitano). Watoto 56,163 wanatarajia kuchanjwa. Kwa chanjo ya kuzuia Polio, watoto watakaochanjwa ni wale wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu. Watoto 34,836 wanatarajia kuchanjwa” alisema Dkt Mahava.
Zoezi la chanjo litafanyika katika vituo vyote 56 vya afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Chanjo itakuwa ikitolewa kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 12:00 jioni siku zote za kampeni ikiwemo Jumamosi na Jumapili” alisema Dkt Mahava kwa msisitizo.
Mganga Mkuu huyo wa Jiji la Dodoma amewataka wananchi wote kujitokeza na kuwapeleka watoto kupatiwa chanjo hiyo muhimu inayotolewa bila malipo.
Kampeni ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua na Polio katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanza tarehe 17/10/2019 na itaendelea hadi tarehe 21/10/2019, ikiongozwa na kaulimbiu isemayo “Chanjo ni kinga, kwa pamoja tuwakinge”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.