Na. Sifa Stanley, DODOMA
MGANGA Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method amewaondoa hofu wanawake wajawazito kuwa chanjo ya UVIKO-19 inayotolewa sasa nchini haina madhara kwao.
Hakikisho hilo alilitoa jana tarehe 6 Agosti, 2021 alipowasilisha mada juu ya tahadhari ya UVIKO-19 katika mkutano wa Baraza la Madiwani alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa viti maalum, Mhe. Khadija Shabani Taya (Keisha) aliyeuliza juu ya usalama wa chanjo ya UVIKO-19 kwa kina mama wajawazito hasa mfumo na ukuaji wa mimba.
Akijibu swali hilo, Mganga mkuu huyo alisema kuwa chanjo hizo ni salama kwa akina mama wajawazito. “Hakuna tafiti zinazoonesha chanjo inapelekea mimba kuharibika” alisema Dkt. Method.
Aidha, alisema kuwa chanjo ya UVIKO-19 kwa baadhi hupelekea maudhi madogo madogo ambayo hutofautiana kati ya mtu na mtu. maudhi hayo ni kama vile homa za usiku, mkono kuvimba, pamoja na kuchoka ambayo huisha ndani ya siku chache baada ya kupata chanjo na kuwaondoa hofu Madiwani akiwahakikishia kuwa chanjo ni salama. “Niwaondoe hofu Waheshimiwa Madiwani, chanjo ni salama, twende tukachanje” alisema Dkt. Method.
Akiongelea suala la umri sahihi wa mtoto kupatiwa chanjo, Mganga Mkuu alisema kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 unaathiri makundi mbalimbali likiwemo kundi la watoto. Alisema kuwa watoto watakaopatiwa chanjo ni wale wenye umri wa miaka mitano na kuendelea. “Watoto wenye umri chini ya miaka mitano hawaathiriki sana na ugonjwa wa UVIKO-19” alisema Dkt. Method.
Aidha, Mganga Mkuu huyo alisema kuwa kwa hivi sasa serikali imeyapa kipaumbele makundi yaliyo katika hali hatarishi zaidi ya kupata maambukizi yaani watumishi wa afya, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 na watu wenye magonjwa sugu.
Vile vile, aliweka wazi kuwa chanjo ya UVIKO-19 haina madhara kwa nguvu za kiume.
Akifafanua zaidi alisema kuwa chanjo haizuii kupata maambukizi ya UVIKO-19, bali wakichanja wengi katika jamii itazuia maambukizi yasiendelee kwenye jamii na inasaidia kupunguza makali ya virusi na vile vile mtu kutopata madhara makubwa ya kiafya endapo atapata maambukizi ya ugonjwa huo, alisema Mganga huyo.
Kuhusu uchukuaji wa tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO-19, alishauri juu ya matumizi ya maji tiririka na sabuni au matumizi ya vitakasa mikono. Pia alishauri wananchi kupata chanjo ili kupunguza kasi ya maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.