UONGOZI wa shule ya msingi Chihoni iliyopo Kata ya Nala, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kuwafundisha wanafunzi somo la uzalendo kwa nchi yao.
Pongezi hizo zimetolewa na Meneja mradi wa Mkoa wa Dodoma kutoka mradi wa Tuimarishe Afya -Health Promotion System Strengthening (HPSS), Kenneth Gondwe, katika hotuba yake kwenye mahafali ya darasa la saba shule ya msingi Chihoni iliyosomwa kwa niaba yake na Dennis Harrison jana.
Gondwe alisema “niipongeze shule ya msingi Chihoni kwa kuwajengea wanafunzi uzalendo kwa nchi yao. Taifa linategemea nini kutoka kwa wanafunzi wahitimu hawa? Taifa linategemea kupata wananchi na wataalam bora watakaolitumikia Taifa lao kwa weledi na uzalendo mkubwa. Uzalendo ni msingi mkubwa wa uwajibikaji katika jamii. Hivyo, wahitimu hawa jamii inawategemea wawe watu wema na wenye moyo wa utoaji huduma kwa viwango bora kabisa ili wawe kielelezo na mfano mzuri kwa shule na jamii kwa ujumla”.
Kuhusu taaluma, aliipongeza shule hiyo kwa kuendelea kuboresh hali ya taaluma na kuitaka kufanya vizuri zaidi. “Ni kweli mnafanya vizuri katika taaluma. Lazima muongeze hali ya ufaulu angalau kufikia asilimia 95 hata 100. Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inatoa elimu msingi bila malipo. Lengo ni kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wanapata elimu hiyo. Zawadi mnayoweza kumpatia ni kufaulu vizuri” alisema Gondwe.
Katika kuhamasisha taaluma na ufaulu kwa wanafunzi, hasa watoto wa kike aliahidi kutoa zawadi. “Napenda kutangaza huwa mwanafunzi wa kike atakayeongoza katika mtihani wa taifa wa kumaliza darasa la saba shuleni hapa, nitamfanyia ‘shopping’ ya vifaa vyote vya shule kwa ajili ya kidato cha kwanza” alisema Gondwe. Vilevile, aliahidi kuchangia mifuko 20 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa choo cha walimu shuleni hapo.Katika risala ya wahitimu kwa mgeni rasmi, iliyosomwa na Sophia Julius, alisema kuwa wamejengewa uzalendo kwa kiwango cha juu. “Tumejengewa uzalendo wa nchi yetu Tanzania toka kwa walimu wetu waliojaliwa wingi wa maarifa na maadili ya kitanzania. Hivyo, taifa litegemee kupata wataalam bora watakaolitumikia kwa hali na mali katika uadilifu wa hali ya juu” alisema Julius.
Julius alisema kuwa wamejengewa madarasa mawili na kupunguza idadi ya wanafunzi waliokuwa wakitumia kivuli cha mtu kwama mbadala wa madarasa. “Pia tumepewa matofali 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matano, hii yote inalenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Tunaipongeza ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma” alisema Julius.
Kuhusu changamoto alizitaja kuwa ni uhaba wa huduma ya maji ambayo yamekuwa yakitoka mara mbili kwa wiki na huduma ya umeme. Changamoto nyingine ni uhaba wa samani za ofisi kwa matumizi ya walimukutokana na kuchakaa kwa samani zilizopo na uhitaji wa ukarabati mkubwa wa madarasa na nyumba za walimu.
Mgeni rasmi aliwatunuku vyeti vya kuhitimu darasa la saba jumla ya wahitimu 83 katika mahafali hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.