Na. Dennis Gondwe, NALA
KIWANDA cha Mbolea cha Itracom kimeajiri wafanyakazi 1,000 wengi wao katika maeneo ya uzalishaji na ujenzi na kusaidia katika kukabiliana na changamoto za ajira kwa vijana.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom, Nduwimana Nazaire alipokuwa akiwasilisha muhtasari wa kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, alipotembelea na kukagua kiwanda hicho katika Kata ya Nala.
Nazaire alisema “kiwanda kina jumla ya wafanyakazi wapatao 1,000. Kati ya hao 380 wana ajira za kudumu na wako moja kwa moja kwenye uzalishaji kiwandani. Idadi ilibaki wako katika Idara ya Ujenzi. Kwa wenye ajira za kudumu kuna watanzania 208 na warundi 172. Baada ya kumaliza usimikaji wa mitambo yote kiwanda, zitatolewa ajira kwa watanzania takribani 2,048 wa kada mbalimbali kufanya kazi kiwandani ili kufikia lengo la uzalishaji wa tani 1,000,000 za mbolea kwa mwaka. Kiwanda cha kuchanganya mbolea kitaajiri takriban watanzania 75. Mtambo wa kuzalisha chokaa utaajiri takribani warundi 10 na watanzania 54. Kiwanda cha kuchakata fosfeti mkoani Manyara, Vilima Vitatu kinachoendelea kujengwa kitaajiri takribani warundi 20 na watanzania 123 wanaofanya kazi katika kiwanda hicho ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023. Hivyo, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2023, kiwanda cha Intracom kitakuwa kimeajiri takribani wafanyakazi 3,067 (warundi 288 na watanzania 2,779).
Akiongelea faida za kiwanda, Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kuwa kiwanda kitakuwa kinazalisha bidhaa za mbolea na virekebishi vya udongo kiasi cha tani 1,500,000 kwa mwaka. Mbolea ya mseto ni 1,000,000, Chokaa Kilimo 300,000 na Mbolea mchanganyiko (blends) 200,000.
Faida nyingine ni wakulima wanapata mbolea kwa bei nafuu ukilinganisha na mbolea nyingine zinazouzwa nchini. Hivyo, kuwapunguzia mzigo wa gharama ya uzalishaji wa bidhaa za kilimo, aliongeza. “Chokaa Kilimo itakayotengenezwa itatumika pia kwa ajili ya kurekebisha tindikali ya udongo (Soil acidity). Hivyo, maeneo yenye udongo wenye tindikali nyingi hususani Nyanda za Juu Kusini na baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa yatafaidika na mbolea na virekebishi vya udongo. Samadi ya wanyama ambayo ni mojawapo ya malighafi muhimu sana katika uzalishaji wa mbolea zetu inanunuliwa kutoka kwa wafugaji wa Dodoma na baadae itatoka katika mikoa ya jirani na nchi nzima. Hii imetengeneza soko ili kuwapatia kipato na ajira wakulima na wafugaji wa ng'ombe wa vijijini nchini Tanzania” alisema Nazaire.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo aliwapongeza wafanyakazi wa kiwanda hicho. Aidha, aliwataka kufanya kazi kwa kujituma, uadilifu na uaminifu na kuwaasa wasijihusishe na vitendo vya udokozi. “Mjitume kutafuta tija ambayo inatakiwa kwa pande zote, kwa muwekezaji na kwetu sisio wafanyakazi. Huwa tunafikiri kinapoharibika, kinaharibika cha mwingine na sisi tunabaki salama. Lakini kikiharibika, sisi ndiyo wakwanza kupata madhara” alisema Chongolo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.