CHAMA cha walimu Tanzania (CWT) kimekabidhi mifuko 300 ya saruji yenye thamani ya shilingi 4,650,000 kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuunga mkono ujenzi wa miundombini ya elimu ya msingi Jijini hapa.
Akikabidhi mifuko hiyo kwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma katika viunga vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania, Mwalimu Deus Seif alisema kuwa moto wa Chama cha Walimu ni Wajibu na Haki. Alisema kuwa Chama cha Walimu kinaamini ili mwalimu afundishe vizuri anahitaji mazingira mazuri ya kufundishia.
“Mwalimu akiingia darasani akakuta darasa zuri halina vumbi, lina sakafu, lina milango mizuri, lina madawati mazuri, Mwalimu atafanya kazi yake kwa raha na weledi. Lakini tunaamini mwalimu akiwa na nyumba nzuri ya kuishi tena karibu na eneo la kazi atafanya kazi nzuri zaidi. Vilevile tunaamini miundombinu ya vyoo si kwa walimu peke yake, hata kwa watoto kwa sababu rasilimali ya Mwalimu ni watoto kwa hiyo na watoto wakiwa katika mazingira yanayovutia kupokea kile anachotoa Mwalimu, Mwalimu atafanya kazi yake kwa amani sana” alisema Mwalim Seif.
Alisema kuwa madarasa yaliyopo katika Halmashauri ya Jiji ni asilimia 37.5, “kwa hiyo na sisi Mstahiki Meya tuwe sehemu ya kutatua changamoto hiyo” aliongeza Mwalim Seif. Mchango huo ni sehemu ya utaratibu wa chama hicho kurudisha shukrani katika jamii na umekuwa ukifanyika nchi nzima, aliongeza.
Kwa upande wake, Afisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Joseph Mabeyo alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaupungufu wa vyumba vya madarasa 1,522, kati ya vyumba vya madarasa 916 vilivyopo, wakati mahitaji ni vyumba 2,438 vya madarasa. Akiongelea nyumba za walimu, alisema kuwa mahitaji ya nyumba za walimu ni 1,777, nyumba zilizopo ni 167 na kuifanya Halmashauri hiyo kuwa na upungufu wa nyumba 1,610. Kufuatia upungufu huo, Halmashauri iliamua kuwashirikisha wadau kuchangia ujenzi wa miundombinu hiyo.
Akipokea mifuko hiyo 300 ya saruji, Mstahiki Meya wa Jiji Dodoma Prof. Davis Mwamfupe alikishukuru Chama Cha Walimu kwa mwitikio wa kuchangia Sekta ya Elimu. Aidha, alitoa wito kwa vyama vya wafanyakazi na wadau wengine kuiga mfano wa Chama cha Walimu kuchangia sekta hiyo yenye mahitaji mengi. Katika kuonesha mfano, alichangia mifuko 10 ya saruji ili iwe hamasa kwa watu wengine katika kuboresha sekta hiyo.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina shule za msingi za serikali 93, zenye jumla ya wanafunzi 97,526.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.