MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ametoa muda wa mwezi mmoja kwa madawati ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyopo katika kila Wilaya kuanza maandalizi ya kuwapanga upya na vizuri wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga kuanzia Jumatatu Septemba 20, hadi Oktoba 18, 2021.
Makalla ametoa tamko hilo jana Septemba 17, 2021 wakati akizindua kitabu cha mpango wa kuwapanga vizuri wafanyabiashara hao Jijini Dar es Salaam.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema uwepo wa Machinga katika maeneo yasiyo umekuwa na athari nyingi ikiwemo kusababisha msongamano wa watu, ajali, kuikosesha Serikali mapato n ahata kukwamisha juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona.
Akifafanua zaidi Makalla amesema mpango huo umewashirikisha wadau wote ikiwamo wafanyabiashara hao, jambo lililowezesha kujua kuwa wapo wafanyabiashara wangapi katika kila wilaya.
Aidha, aliyataja makundi matano ambayo mpango huo utawagusa kuwa ni wafanyabiashara waliojenga vibanda juu ya mifereji na mitaro, wale walio mbele ya maduka ya watu ambao husababisha wateja kushindwa kuingia na kutoka dukani.
Makundi mengine ni wafanyabiashara waliopo katika hifadhi za barabara, wanaofanya biashara na kuzuia njia za waenda kwa miguu, hali ambayo husababisha baadhi ya wapita njia kugongwa na magari kutokana na kulazimika kupita barabarani kabisa na pia wanaofanya biashara mbele ya taasisi za umma kama vile shule za msingi na sekondari, aliongeza Mhe. Makalla.
Vilevile, ameiagiza ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuendelea kuweka mabango ya katazo ya kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.
Ameagiza pia kila Mkuu wa Wilaya kuhakikisha madawati ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yanaratibu wamachinga hao bila bughudha.
Naye mwakilishi wa Wamachinga, Steven Lusinde ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania, amesema kuwa utaratibu huo wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine nchini.
“Tumepokea agizo lako, tutalifikisha kwa wenzetu kama lilivyo ili kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Wakuu wa Wilaya. Tunaomba Wakuu wa Wilaya wazingatie hili kwamba kutupanga upya na kutupanga vizuri, kwa sababu kuna maeneo wanastalihi kutupanga vizuri maana tupo maeneo sahihi na si upya” alisema kiongozi huyo.
Lusinde alikiri kuwa ni kweli wamachinga wamekiuka utaratibu kwa kufanya biashara maeneo yasiyo rasmi.
“Niwaombe wanzangu popote walipo nikiwa kama Makamu Mwenyekiti wa Machinga Tanzania kwamba kwa maelekezo haya tuwe watulivu tuhakikishe tunajianga vizuri” alimalizia Lusinde.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.