Imeelezwa kuwa kujengwa kwa daraja la mto Hurui lenye urefu wa mita 30 lililopo katika kijiji cha Hurui kata ya Kikore wilayani Kondoa mkoani Dodoma limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi waliokuwa wanapata adha ya muda mrefu ya usafiri kutokana na kukosekana kwa daraja baada ya daraja la awali kusombwa na maji ya mvua.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa daraja la Hurui wilayani Kondoa. Uwekaji wa jiwe la msingi umefanywa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Amesema kama yalivyo maelekezo ya Mhe. Rais kuhakikisha vijiji vyote vinapitika kwa barabara, katika kipindi cha miaka mitatu (3) ya Rais Samia zaidi ya bilioni 7 na milioni 200 zimetolewa katika Wilaya ya Kondoa kwaajili ya ujenzi wa barabara na madaraja.
Pia ameongeza kuwa wao kama OR- TAMISEMI wamepokea maagizo ya Makamu wa Rais kuanza kujenga barabara ya
Ntundwa-Hurui yenye urefu wa Km 46.8 ili wananchi waweze kuzifikia huduma za kijamii na waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi wakati wote.
Vile vile Dkt. Dugange amempongeza Mhandisi Victor Seff kwa usimamizi mzuri wa fedha na ujenzi bora wa miundombinu ya barabara na madaraja za wilaya.
Naye Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amesema usanifu wa daraja umefanywa na wahandisi wa ndani chini ya Kitengo cha "TARURA Engineering and Environmental Consultanting Unit" na ujenzi umefanywa na Mkandarasi M/S Madata Investment Company Limited. Utekelezaji wake umefikia asilimia 95 kukamilika na daraja lina uwezo wa kubeba magari uzito wa tani 70 na litadumu kwa zaidi ya miaka 100.
"Daraja hili linaenda kuondoa changamoto ya mawasiliano kwa tarafa za Pahi na Bereko wilayani Kondoa pia barabara inayotumika mpaka kufikia daraja hili inaunganisha barabara kuu kutoka Dodoma kwenda Babati", amesema.
Bw. Iddi Malatu mkazi wa kijiji cha Madege Kata ya Kikole ameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja la mto Hurui kwani limewasaidia wananchi kusafiri na kusafirisha mazao yao na kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.
"Daraja hili lilipoharibiwa na maji ya mvua tangu mwaka 2019 wananchi wa maeneo haya tulikuwa tukipata shida kuvuka kwenda ng'ambo ya pili kutokana na mto huu kujaa maji ambapo ilipelekea wanafunzi kushindwa kwenda shule pia hata wajawazito walikuwa wanajifungulia njiani kwa kushindwa kwenda zahanati iliyopo upande wa pili, kwakweli daraja hili ni mkombozi sana kwetu", alisema.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.