WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa,(OR-Tamisemi), Angellah Kairuki ameitaka Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) kubuni mikakati ya kuboresha huduma ya usafiri ndani ya Jiji la Dar es Salaam na kupanua wigo wa huduma hiyo katika majiji mengine yanayokidhi vigezo.
Wito huo ameutoa leo Novemba 15, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa DART na kuwataka kuweka mikakati ya utoaji wa huduma hiyo katika Majiji ambayo yanakidhi vigezo ili kutoa huduma hiyo nchi nzima
Amesema kuwa wakati wa uanzishwaji wa Wakala huo ulikuwa ni kwa Jiji la Dar-es-salaam lakini bado kuna majiji mengine ambayo yanatamani kupata huduma ya mabasi yaendayo kwa haraka, na kuwataka kuweka nguvu kulifanikisha hilo.
Akizungumzia hoja za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG),Kairuki ameitaka bodi hiyo kuhakikisha hoja zote za ukaguzi zinajibiwa kwa wakati na kuzifunga na kuhakikisha hakuzalishwi hoja nyingine.
“Sitegemei tunapoenda kwenye ukaguzi wa mwaka 2021/2022 na kaguzi nyingine mbeleni kupata hoja zinazojirudia wakati mlishajifunza hoja zipi ambazo huwa zinajitokeza wakati kuna wahasibu wabobezi, wakaguzi wa ndani wazoefu na wataalam wengine, hivyo wekeni mkazo kwenye eneo hilo” amesisitiza Waziri Kairuki
Kwa upande wa Matumizi ya TEHAMA, Kairuki ameitaka bodi ya Wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia matumizi ya mifumo hasa katika suala zima la matumizi ya Kadi za kielektroniki ifikapo Februari, 2023 na pia kuangalia ubora wa kadi zenye viwango na ambazo hazitaweza kugushiwa.
Amewataka kuhakikisha mikataba inapitiwa ili kujua masharti ya mikataba iliyopo, ambayo imepitwa na wakati lengo ni kuhakikisha huduma bora inatolewa na upatikanaji wa faida inayopatikana.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.