MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza kazi ya uchimbaji wa visima zaidi ili kuongeza uzalishaji wa maji mjini kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya ukame.
Kauli hiyo imetolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa viongozi wa DAWASA alipokutana nao pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Waziri wa Maji kwa lengo la kujadili hali ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Amesema kuwa Serikali itahakikisha maeneo yote yanapata huduma za maji na kuongeza kuwa kazi ya uchimbaji wa visima pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya maji inaendelea ili kufikia matamanio ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikisha huduma ya maji karibu na makazi ya wananchi.
Mara baada ya kukagua na kuwasha pampu katika mradi wa Visima vya Maji Kigamboni, amesema kuwa visima hivyo vinauwezo wa kuzalisha lita milioni 70 za maji kwa siku vitakavyosaidia katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Mnamo Novemba Mosi Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia alimuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhakikisha anasimamia uunganishwaji wa maji kutoka Kigamboni kuja maeneo ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na kuangalia maunganisho ya ili kukabiliana na uhaba wa maji.
Waziri Mkuu amesema kuwa mahitaji ya maji kwa Dar es Salaam na Pwani ni lita milioni 544 kwa siku, na ambapo DAWASA inazalisha maji lita milioni 520 kwa siku, mbadala wa maji ya visima hasa kwa kipindi hiki ni jambo la msingi sana kwa lengo la kukabiliana na upungufu wa maji.
"Katika kipindi hiki ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kimepungua, uzalishaji wa maji nao umepungua na kufikia lita milioni 300 kwa siku, na kusababisha upungufu wa lita milioni 244, hivyo lita milioni 70 zinazoingizwa mjini kutoka katika mradi wa Visima vya Kigamboni, kutakuwa na upungufu wa maji lita milioni 174, hivyo zitasaidia kupunguza changamoto ya maji katika baadhi ya maeneo", alisema Majaliwa
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.