Na. Sifa Stanley, DODOMA.
VIONGOZI wa Kata pamoja na wadau mbalimbali wa mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wapatiwa elimu ya chanjo ya UVIKO-19 na kuhimizwa kuchanja chanjo hiyo.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri katika kikao kazi cha wadau wa usafi wa mazingira kilichofanyika katika ukumbi Polisi Jamii, wakati akihamasisha viongozi kupata kupata chanjo ya UVIKO-19.
Shekimweri aliwahakikishia viongozi na wadau hao kuwa chanjo ni salama, haina madhara kiafya na inatolewa kwa hiari, hivyo kuwaomba viongozi hao wapate elimu ya chanjo kisha waende kuchanja ili kujikinga dhidi ya UVIKO-19.
Akielezea kuridhishwa na mwitikio wa viongozi wa dini katika hatua za kujikinga na ugonjwa huo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa viongozi wa dini wanashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19, kwa kuzingatia kanuni za afya za kujikinga na ugonjwa huo.
“Niwashukuru viongozi wa dini, mnazingatia kanuni za afya, nimepita katika makanisa kuomba ushirikiano wa kupambana na ugonjwa huu mwitikio ni mzuri na kanuni za afya zina zingatiwa” aliongeza.
Naye Afisa Afya wa Jiji, Abdalah Mahiya, aliwapatia washiriki wa mkutano huo elimu ya ugonjwa wa UVIKO-19, ambapo aliwaelezea namna ugonjwa huo unavyoambukizwa na kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Pia aliwaeleza njia bora za kujikinga na ugonjwa huo ambazo ni kuzingatia kanuni za afya pamoja na kupata chanjo ya ugonjwa huo na kuwahakikishia kuwa chanjo ni salama.
“Chanjo ya korona ipo, na ni aina ya Jonhson Johnson ambayo imefanyiwa uchunguzi wa kisayansi na kuthibitishwa na kupitishwa na Shirika la Afya Dunuani (WHO) kuwa ni salama, pia imepita katika wizara ya afya ya nchi yetu na kuthibitisha usalama wake” alisema Mahiya”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.