Na Sifa Stanley na Getruda Shomi
VIJANA wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wajitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 katika kituo cha Afya Makole ikiwa ni mwitikio wao baada ya kuhamasishwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri.
Vijana hao 30 walionesha mwitikio huo baada ya kuhamasishwa juu ya chanjo na usalama wake na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipofanya ziara na kuzungumza na wafanyabiashara wa soko la Sabasaba jijini hapa.
Shekimweri aliwahakikishia usalama wa chanjo hiyo na kuwaeleza kwamba hata yeye ameshapata chanjo. Aliwataka wananchi kuondoa hofu na kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ambayo inatolewa bure na kwa hiari.
Mkuu wa Wilaya alivitaja vituo vinavyotoa chanjo ya UVIKO-19 katika Wilaya ya Dodoma kuwa ni Kituo cha Afya Makole, Kituo cha Afya Hombolo, Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma (General), Hospitali ya St. Gema, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya DCMC. “Mimi jana nimechanja, sijapata kadhia yoyote, nimeshinda salama, nimelala salama, na kazi inaendelea” alisema Shekimweri.
Aidha, aliwataka wakazi wa Jiji la Dodoma kupuuza taarifa za upotoshaji katika mitandao ya kijamii na kufuata taarifa na maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya. Baadhi ya mitandao inatoa taarifa zisizo sahihi na za kupotosha kwa sababu watu wengi hujifanya wataalamu wa afya, aliongeza.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wafanyabiashara kuzingatia kanuni za kujikinga na UVIKO-19 kwa kuhakikisha maji tiririka na sabuni yanakuwepo katika maeneo yao ya biashara. Alisema kuwa iwapo maji tiririka na sabuni havitakuwepo katika maeneo ya biashara watazuiliwa kufanya biashara zao. “Kufikia kesho ikiwa hakuna maji tiririka, sabuni na vitakasa mikono, tutawazuia shughuli hizo kwa lengo la kuokoa maisha yenu na wananchi wengine” alisisitiza Shekimweri.
Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma aliwataka askari wa usalama barabarani kusimamia sheria ikiwemo daladala kutokusimamisha abiria ili wawe sehemu ya mapambano ya UVIKO-19.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.