MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi ameagiza apatiwe orodha ya majina ya taasisi zote katika Wilaya hiyo zinazokaidi kulipa tozo ya uzoaji taka kwa ajili ya usafi wa mazingira hali inayopelekea kuhatarisha afya za wakazi wa Jiji.
Katambi aliyeongozana na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizindua kituo cha kupokelea mifuko ya plastiki katika Kata ya Uhuru leo asubuhi.
"Tuna wajibu wa kuhakikisha mazingira yanakuwa salama, zipo taasisi ambazo hazilipi tozo ya uzoaji taka...naomba orodha ya majina ya taasisi zote zinazokaidi kulipia tozo ya taka kwani haiwezekani uchafue wewe mazingira, kisha kipindupindu tuugue sisi” alisema.
Vilevile, aliwataka watendaji kuwasimamia wananchi katika maeneo yao ili kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi na kwa wanaokaidi kufanya usafi katika maeneo yao au kulipa tozo za kuzolea taka orodha yao iwasilishwe kwake.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema “agenda ya mifuko ya plastiki ni sehemu ya agenda yetu, vyombo vyote vichukue hatua kali bila kumvumilia mtu kwani mifuko ya plastiki imekuwa na athari kubwa katika mazingira ikiwemo kuziba mifereji ya maji na kusababisha uchafu kuzagaa na mafuriko na kusababisha vifo kwa mifugo pindi wanapokula mifuko hiyo" alisema.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa jiji lake litaongoza katika kampeni ya upigaji marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, jiji la Dodoma tunaenda kuongoza na kuwa wa mfano Tanzania. Tumekuwa na utamaduni wa kuongoza katika mapato, usafi, afya, elimu, sababu kubwa sisi wote ni vijana. Tunafikiria miaka 50 ijayo ya siyo miaka 50 iliyopita” alisema Kunambi. Aidha, aliwapongeza wakazi wa jiji la Dodoma kwa utulivu na ushirikiano wanaoendelea kumpatia katika kutekeleza majukumu yake.
Kunambi aliwataka wakazi wa jiji hilo kutii sheria bila shuruti na kusema kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mtu. Katika nyumba yako au eneo unalofanyia shughuli zako, hakikisha hakuna mfuko wa plastiki unaozagaa, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria, aliongeza.
Mkurugenzi wa jiji alieleza masikitiko yake kwa baadhi ya taasisi zinazokwamisha juhudi za usafi wa mazingira kwa kukataa kulipa tozo za uzoaji taka katika maeneo yao. “Wengine wanafikiria usafi siyo sehemu yao. Zipo taasisi kubwa hazilipi tozo ya usafi wa mazingira. Tusimame pamoja ili kusafirsha jiji letu” aliongeza Kunambi.
Nae mkuu wa idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu katika Halmashauri ya jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa Halmashauri hiyo ilijikita katika kutoa elimu kuanzia ngazi ya mtaa, kata na wilaya juu ya katazo la serikali la matumizi ya mifuko ya plastiki na kuelezea mifuko mbadala. Alisema kuwa elimu hiyo ilitolewa kwa njia ya redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii, matangazo mbalimbali na kupitia taasisi kama shule na maeneo ya masoko ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.