MKUU mpya wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remedius Emmanuel ameapishwa rasmi mwanzoni mwa juma hili Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka ili kuanza kuiongoza Wilaya hiyo iliyo miongoni mwa Wilaya saba zinazounda Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya Nchi.
Akitoa shukurani zake mbele ya Mkuu wa Mkoa na hadhara iliyohudhuria hafla ya uapisho huo Mhe. Emmanuel alisema, “Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kupata nafasi hii, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kuwa miongoni mwa vijana wachache katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuniteua na kuniamini kuwa Mkuu wa Wilaya nitayoiongoza na kumuwakilisha katika ardhi ya Wilaya ya Kongwa, Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani hiyo;
Kazi yangu ni moja kubwa kabisa kwenda kutekeleza ile imani ambayo Mheshimiwa Rais ameionesha kwangu kama kijana na hivi karibuni alisema atachagua vijana, na mimi ni miongoni mwa hao vijana. Kazi yangu ni moja, kuhakikisha yale aliyoyaahidi, dira ya Mheshimiwa Rais, maono ya mheshimiwa Rais, matarajio ya mheshimiwa Rais, mategemeo ya Mheshimiwa Rais, mategemeo ya Mheshimiwa Rais kwenda kuyatekeleza katika Wilaya ya Kongwa” alisema DC Emmanuel kwa kujiamini.
Mkuu huyo wa Wilaya alimshukuru pia Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Mtaka na kumuahidi ushirikiano mkubwa huku akikumbusha kuwa tangu Mkuu huyo ameanza kuongoza Mkoa wa Dodoma tayari ameshatoa maelekezo na kuonesha dira ya mkoa wa Dodoma, hivyo atashirikiana naye katika kutekeleza malengo mkoa kwa kuwa Kongwa ni sehemu ya mkoa wa Dodoma.
Hafla ya kuwaapisha wakuu wapya wa Wilaya ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo wakuu wa Wilaya zingine za Mkoa wa Dodoma, Wakurugenzi, viongozi wa Dini na wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.