WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewapa muda wa mwezi mmoja viongozi wa mikoa na halmashauri wawe wamekutana na wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga na kupanga namna bora ya usimamizi wa shughuli za biashara ikiwemo kutenga maeneo ya kufanyia biashara zao.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akizindua mpango wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, ambapo aliwataka Wakuu wa Mikoa wawe makini katika zoezi la kuwapanga Wamachinga nchini na kuepuka vurugu, fujo na uonevu.
Mhe. Majaliwa aliitoa kauli hiyo jana Jumatano, Septemba 15, 2021 wakati akizungumza kwa njia ya video na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Waziri wa Viwanda na Biashara, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Uongozi wa Wamachinga.
Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya waone namna ya kutumia baadhi ya barabara za katikati ya majiji na miji kufungwa muda wa alasiri ili kuruhusu Wamachinga kufanya biashara zao katika barabara hizo. “Hii ni fursa nzuri kwa wajasiriamali wetu kufanya shughuli zao.”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.