MADIWANI Halmashauri ya Manispaa ya Songea wamefanya ziara katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma lenye lengo la kujifunza juu ya uanzishwaji na uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo bustani ya mapumziko Chinangali, Dodoma City Hotel, na jengo la kitega uchumi la Government City Compex lililopo ndani ya mji wa Serikali Mtumba jijini humo.
Madiwani hao wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Maiko Mbano ambaye ni Diwani wa Kata ya Msalamala, walitembelea miradi hiyo wakiwa wameambatana Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema kwenye ziara yao ya siku moja iliyolenga kujifunza kutoka kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma namna Jiji linavyojiendesha na mafanikio yake katika kuendesha miradi mikubwa kwa kutumia mapato ya ndani.
Aidha, mafunzo hayo yalilenga kujifunza namna Jiji linavyokusanya mapato yake, namna ya udhibiti wa taka na usafi, utekelezaji wa miradi kwa mapato ya ndani, namna Jiji linavyofanya kazi katika kitengo chake cha Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF) pamoja na mipango miji.
Akiwakaribisha Madiwani hao Naibu Meya wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Emmnuel Chibago alisema kuwa, ni faraja kubwa kwa jiji kupata wageni ambao ni viongozi wa Halmashauri nyingine kuja kubadilishana uzoefu.
Chibago alisema Jiji la Dodoma limekuwa likipata wageni wa aina hiyo mara kwa mara kutokana na hatua kubwa waliyopiga katika kutekeleza miradi mikubwa hususani inayojengwa kwa mapato ya ndani ikiwemo mahoteli.
“Tutawatembeza katika miradi yetu mikubwa ambayo tunaiendesha kwenye Halmashauri yetu, ipo iliyokamilika na mingine inaendelea kujengwa” alisema Naibu Meya huyo.
Awali kabla ya kutembelea miradi jijini, madiwani hao walipewa taarifa za idara kadhaa ikiwemo Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu iliyowasilishwa na Afisa Mazingira, Ally Mfinanga, Mipango Miji iliyowasilishwa na Epifania Komba, Mipango Takwimu na Ufuatiliaji iliyowasilishwa na Rukia Bakari, pamoja na taarifa ya hali ya uandikishaji bima ya afya ya Jamii iliyoboreshwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.