MKUU wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi kwa pamoja wamemaliza na kuhitimisha migogoro ya Ardhi ya muda mrefu katika Kata mbili za Kikuyu Kusini na Kikuyu Kaskazini Jijini Dodoma ambapo wananchi wote waliothibitika kuhusika na maeneo yaliyokuwa na migogoro watapatiwa viwanja mbadala na vya bei nafuu vilivyopimwa na Jiji hilo kwa ajili ya makazi.
Baada ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mgogoro huo, wakazi wapatao 233 katika Kata ya Kikuyu Kusini watapatiwa viwanja mbadala na wakazi 458 wa Kata ya Kikuyu Kaskazini waliothibitika kuvamia eneo lililokuwa la msitu watapatiwa viwanja vya bei nafuu, huku wakazi wapatao 15 wa Kata hiyo wakipatiwa viwanja mbadala bure.
Wakazi hao wanadaiwa kuvamia maeneo yaliyokuwa yamehifadhiwa yakiwemo ya misitu na barabara na kuanzisha makazi na shughuli za kiuchumi kwa miaka kadhaa, lakini Halmashauri ya Jiji hilo imeamua kuwapa viwanja vilivyopimwa kama sehemu ya kuwasaidia wakazi wake na kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika Kata hizo.
Viongozi hao kwa pamoja walifanya mikutano ya hadhara katika Kata hizo jana Aprili 2, 2019 na kuzungumza na wakazi wa Kata hizo, ambao walikuwa na malalamiko ya kuondolewa katika maeneo wanayodaiwa kuvamia kinyume na sheria.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Kunambi aliwashauri wakazi hao kutouza viwanja wanavyopewa kama fidia badala yake waviendeleze kwani baada ya kila muhusika kupewa kiwanja chake, Halmashauri haitegemei kusikia mgogoro wowote au madai yanayohusiana na viwanja kutoka kwenye maeneo hayo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya pamoja na wananchi, baada ya zoezi la kuwapa viwanja mbadala wahusika hawa, sitegemei kusikia mgogoro tena katika Kata hii, suala hili leo tunalifunga rasmi…nawashauri msiuze viwanja vyenu tutakavyowapa bali mviendeleze kwa manufaa yenu na watoto wenu” alisema Kunambi.
Kunambi alisema Halmashauri imetenga takribani viwanja 5,000 vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 7 kwa ajili ya kuvitoa bure kama fidia kwa wananchi kwa maeneo yenye migogoro sugu ya Ardhi Jijini humo, na kwamba mpango huo ndiyo suluhisho la migogoro yote ya Ardhi katika Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Katambi aliwatahadharisha wakazi wa Wilaya hiyo kuacha tabia ya kuhamasishana kuvunja sheria kwa vigezo vya kudai haki vinginevyo wafuate taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi.
Akizungumza na wakazi wa Kata hizo, Katambi alisema kumekuwa na baadhi ya watu wanaoshawishi wenzao kuvunja sheria na kuvuruga amani bila sababu ya msingi na kwamba Serikali haitawavumilia endapo hawataacha tabia hiyo.
Alisema awali alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mwaka 2018, alifanya ziara katika Kata hizo mbili za Kikuyu Kusini na Kaskazini Mwezi Septemba ambapo alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji kupeleka timu ya wataalam wa Ardhi ili wafanye uchunguzi wa kina wa migogoro iliyopo ili kupata ufumbuzi.
“Ripoti ya kina kuhusu mgogoro wa hapa Kikuyu Kusini imekamilika na Mkurugenzi ameshanikabidhi hii hapa mikononi mwangu, inaeleza kila kitu…nyinyi wote mlivamia eneo la Serikali na hakuna hata mmoja mwenye nyaraka za umiliki za eneo hilo…Mkurugenzi anafanya hisani tu kuwapa viwanja mbadala kwa sababu Serikali ya awamu ya tano inajali wananchi wanyonge” alisema Katambi huku akiwaonesha wakazi hao ripoti ya uchunguzi wa mgogoro huo.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwaeleza wakazi hao kuwa, Mkurugenzi wa Jiji na wataalam wake wa Ardhi wamefanya kazi nzuri katika hatua zote za kuchunguza mgogoro huo kwani ripoti imeainisha kila kipande cha Ardhi kinacholalamikiwa na mmiliki wake amepigwa picha kama sehemu ya vielelezo vya msingi.
Viongozi hao wa Wilaya ya Dodoma wako katika ziara ya kutembelea maeneo yenye migogoro ya Ardhi ili kuhakikisha inamalizika kabisa katika Jiji la hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.