Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri aliwataka wakuu wa shule na walimu wakuu kutekeleza mpango wa huduma ya chakula kwa wanafunzi wote shuleni ili kuhakikisha wanapata lishe bora jambo litakalopelekea kujifunza kwa ufanisi.
Aliyasema hayo ofisini kwake wakati akihamasisha wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuandikisha watoto shuleni katika ngazi ya awali na msingi pia wale wanaojiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2025.
Akisisitiza kuhusu mpango wa huduma ya chakula kwa wanafunzi shuleni, “……kuna uhusiano mkubwa sana kati ya ufaulu na lishe, mtoto ambaye hajashiba ni ngumu sana kumsikiliza mwalimu akamuelewa na akazingatia, ni tofauti na mtoto aliyepata chakula shuleni” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wa wazazi na walezi katika Jiji la Dodoma walisema kuwa wamepokea vizuri mpango wa huduma ya chakula kwa wanafunzi shuleni ili kuhakikisha wanapata lishe bora ikiwa ni chachu ya maendeleo ya wanafunzi kiujumla.
Charles Maganya, mzazi kutoka Kata ya Ihumwa alisema kuwa mpango huo kama utatekelezwa vizuri utasaidia katika maendeleo ya watoto wawapo shuleni kwa sababu ili mtoto ajifunze ni lazima awe ameshiba na kuwa imara kimwili na kiakili. “Ni mpango mzuri na umepokelewa vizuri. Mpango huu kwa namna moja utakuwa ni chachu kubwa ya maendeleo ya watoto wetu shuleni kwa sababu watapata nafasi ya kusoma bila shida wakiwa wameshiba” alisema Maganya.
Akiongelea kuhusu kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora shuleni, mkazi wa Kata ya Ipagala, Bathseba Njigo, alifafanua kuwa wao kama wazazi wanahakikisha wanaunga mkono jitihada hizo kwa kuchangia vyakula shuleni ili kuhakikisha watoto wanakaa darasani wakiwa wameshiba tayari kwa kupokea kile wanachofundishwa na walimu. “Uzuri ni kwamba shule nyingi zina utaratibu wa kuchangia chakula, sisi kama wazazi kwa nafasi yetu sehemu kubwa tunajitahidi kuunga mkono hizo jitihada ili watoto waweze kukaa darasani wakiwa wameshiba, waweze kupokea kile walimu wanachowapatia” alisema Njigo.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya wazazi hupuuzia jambo hilo wakidhania kuwa ni michango isiyokuwa na ulazima. Alisema kuwa wazazi hao hawawatendei haki watoto wao na wadau wengine wa elimu wanaoweka jitihada katika kuboresha elimu, ufaulu wa wanafunzi na taifa kwa ujumla.
Nae, mkazi wa Kata ya Ihumwa, Esther Yohana, aliwashauri wazazi na walezi kujitoa ipasavyo katika kuchangia vyakula na michango mingine kwa wanafunzi ili kuimarisha mpango wa lishe bora shuleni kwa sababu ni faida kwa wanafunzi, wazazi na taifa kwa ujumla. “Wazazi tuchangie kwa sababu ni faida watoto wetu na kwa taifa letu” alisema Yohana.
Wazazi, walimu na wadau wote wa elimu nchini wanatakiwa kushirikiana ipasavyo katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mahitaji muhimu shuleni ikiwemo elimu bora na lishe bora ili kuimarisha afya zao kimwili na kiakili kwa lengo la kutengeneza nguvu kazi ya taifa imara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.